Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 20:20-29 Biblia Habari Njema (BHN)

20. Lakini mfalme wa Edomu akasisitiza: “Hatutawaruhusu.” Mara, Waedomu wenye nguvu wakatoka kupigana nao.

21. Basi, Waedomu wakakataa kuwapa ruhusa Waisraeli kupita katika mipaka yao. Waisraeli wakageuka na kushika njia nyingine.

22. Waisraeli wote walisafiri kutoka Kadeshi, wakafika kwenye Mlima Hori.

23. Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni huko kwenye Mlima Hori, mpakani mwa nchi ya Edomu,

24. “Aroni atakufa; hataingia katika nchi ambayo nimewapa watu wa Israeli kwa sababu nyinyi wawili mliiasi amri yangu kule Meriba

25. Mchukue Aroni na Eleazari mwanawe, uwalete juu ya Mlima Hori.

26. Kisha, mvue Aroni mavazi yake rasmi, umvalishe mwanawe Eleazari. Aroni atakufa akiwa huko mlimani.”

27. Mose alifanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Wote watatu walipanda mlimani mbele ya jumuiya yote ya watu.

28. Kisha Mose alimvua Aroni mavazi yake rasmi, akamvalisha mwanawe, Eleazari. Naye Aroni akafa palepale mlimani. Kisha Mose na Eleazari wakateremka chini.

29. Jumuiya yote ya watu ilipopata habari kwamba Aroni amefariki, ikafanya matanga ya siku thelathini.

Kusoma sura kamili Hesabu 20