Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 20:11-22 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Kisha Mose akainua mkono wake, akaupiga ule mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika kwa wingi, watu wakanywa pamoja na mifugo yao.

12. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, “Kwa kuwa nyinyi hamkuniamini mimi, wala kunistahi mbele ya macho ya Waisraeli, basi kwa sababu hiyo hamtaiingiza jumuiya hii katika ile nchi niliyowapa.”

13. Hayo ni maji ya Meriba, mahali ambapo Waisraeli walimnungunikia Mwenyezi-Mungu, naye alijionesha kwa utakatifu kati yao.

14. Mose alipeleka wajumbe kutoka Kadeshi kwa mfalme wa Edomu akamwambia: “Ndugu yako, Israeli, asema hivi: Wewe wazijua taabu zote tulizozipata.

15. Jinsi babu zetu walivyokwenda Misri, ambako tuliishi kwa muda mrefu na jinsi Wamisri walivyowatesa babu zetu, wakatutesa na sisi pia.

16. Tulimlilia Mwenyezi-Mungu, naye akakisikia kilio chetu, akatuletea malaika aliyetuondoa Misri. Sasa tuko hapa Kadeshi, mji unaopakana na nchi yako.

17. Tafadhali uturuhusu tupite nchini mwako. Hatutakanyaga mashamba yenu, wala yale ya mizabibu; wala hatutakunywa maji ya visima vyenu. Tutaifuata barabara kuu ya mfalme na kwenda moja kwa moja bila kugeuka kulia au kushoto, mpaka tutakapotoka katika nchi yako.”

18. Lakini mfalme wa Edomu akamjibu, “La! Hutapita katika nchi yangu, kama ukipita nitatoka na kukushambulia kwa upanga.”

19. Waisraeli wakamwambia, “Sisi tutafuata njia kuu; kama sisi na mifugo yetu tukinywa maji yenu, tutalipa. Tunachoomba tafadhali turuhusu tu, tupite kwa miguu wala hatutaki neno lolote lingine.”

20. Lakini mfalme wa Edomu akasisitiza: “Hatutawaruhusu.” Mara, Waedomu wenye nguvu wakatoka kupigana nao.

21. Basi, Waedomu wakakataa kuwapa ruhusa Waisraeli kupita katika mipaka yao. Waisraeli wakageuka na kushika njia nyingine.

22. Waisraeli wote walisafiri kutoka Kadeshi, wakafika kwenye Mlima Hori.

Kusoma sura kamili Hesabu 20