Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 16:28-41 Biblia Habari Njema (BHN)

28. Hapo Mose akawaambia watu, “Hivi ndivyo mtakavyotambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyenituma kufanya mambo haya yote, wala siyo kwa matakwa yangu mwenyewe.

29. Watu hawa wakifa kifo cha kawaida, au wakipatwa na maafa kama watu wengine, basi jueni kuwa Mwenyezi-Mungu hakunituma.

30. Lakini Mwenyezi-Mungu akifanya jambo ambalo halijapata kutendeka, ardhi ikafunuka na kuwameza watu hawa pamoja na kila kitu chao, wakaenda kuzimu wakiwa hai, basi mtajua kuwa watu hawa wamemdharau Mwenyezi-Mungu.”

31. Mara tu alipomaliza kusema maneno hayo yote, ardhi chini ya Dathani na Abiramu ikafunuka

32. kuwameza watu hao, jamaa zao, pamoja na wafuasi wote wa Kora na mali zao zote.

33. Basi, wao, pamoja na vyote vilivyokuwa vyao wakashuka kuzimu hali wangali hai. Ardhi ikawafunika, wote wakatoweka.

34. Waisraeli wote wengine waliokuwa karibu waliposikia vilio vyao walikimbia wakisema, “Tukimbie, ardhi isije ikatumeza na sisi pia.”

35. Kisha Mwenyezi-Mungu akapeleka moto ukawateketeza wale watu 250 waliokwenda kufukiza ubani.

36. Baada ya hayo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

37. “Mwambie Eleazari mwana wa kuhani Aroni avitoe hivyo vyetezo penye moto, akautapanye mbali moto uliomo ndani, maana vyetezo hivyo ni vitakatifu.

38. Vimekuwa vitakatifu kwa sababu watu hawa walivileta madhabahuni pa Mwenyezi-Mungu. Basi, vichukue vyetezo vya watu hao waliouawa kwa sababu ya dhambi zao, vifuliwe kuwa vyembamba ili viwe kifuniko cha madhabahu. Hili litakuwa onyo kwa Waisraeli wote.”

39. Basi, kuhani Eleazari alivichukua vyetezo hivyo vya shaba ambavyo vililetwa mbele ya Mwenyezi-Mungu na wale watu walioteketezwa vikafuliwa kuwa kifuniko cha madhabahu.

40. Hili lilikuwa onyo kwa Waisraeli kwamba mtu yeyote ambaye si kuhani, yaani asiye wa ukoo wa Aroni asiende madhabahuni kumfukizia Mwenyezi-Mungu ubani. La sivyo ataangamizwa kama Kora na wafuasi wake. Haya yote yalitendeka kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Eleazari kwa njia ya Mose.

41. Kesho yake, Waisraeli wote walimnungunikia Mose na Aroni wakisema, “Mmewaua watu wa Mwenyezi-Mungu.”

Kusoma sura kamili Hesabu 16