Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 16:15-27 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Mose alikasirika mno, akamwambia Mwenyezi-Mungu “Usizikubali sadaka za watu hawa. Mimi sijachukua punda wa mtu yeyote, wala sijamdhuru mtu!”

16. Mose akamwambia Kora, “Kesho usikose kuja pamoja na wafuasi wako mbele ya Mwenyezi-Mungu. Aroni pia atakuwapo.

17. Kila mmoja wenu achukue chetezo chake, na kutia ubani, kisha atakipeleka mbele ya Mwenyezi-Mungu; kwa jumla vitakuwa vyetezo 250; wewe pia na Aroni, kila mmoja atakuwa na chetezo chake.”

18. Basi, kila mmoja wao akachukua chetezo chake, akatia makaa ya moto na ubani, kisha wakaenda na kusimama mlangoni mwa hema la mkutano, pamoja na Mose na Aroni.

19. Naye Kora akawakusanya watu wote pamoja, wakasimama mbele ya Mose na Aroni ambao walikuwa mlangoni mwa hema la mkutano. Ndipo utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukawatokea watu wote!

20. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni,

21. “Jitengeni na watu hawa, niwaangamize sasa hivi.”

22. Lakini Mose na Aroni wakajitupa chini kifudifudi na kusema, “Ee Mwenyezi-Mungu uliye asili ya uhai wa binadamu wote. Je, mtu mmoja akikukosea, utaikasirikia jumuiya nzima?”

23. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

24. “Waambie watu waondoke karibu na makao ya hema ya Kora, Dathani na Abiramu.”

25. Basi, Mose akaenda kwa Dathani na Abiramu, akifuatwa na wazee wa Israeli.

26. Alipofika, akawaambia watu, “Tafadhalini ondokeni kwenye hema za watu hawa waovu na msiguse kitu chao chochote, msije mkaangamizwa pamoja nao kwa sababu ya dhambi zao zote.”

27. Watu wakaondoka kwenye makao ya Kora, Dathani na Abiramu.Dathani na Abiramu wakatoka mahemani mwao na kusimama mlangoni wakiandamana na wake zao na watoto wao wote hata wale wanaonyonya.

Kusoma sura kamili Hesabu 16