Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 16:11-22 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Kwa hiyo wewe na kundi lako mnamshambulia Mwenyezi-Mungu. Nyinyi mnamnungunikia Aroni, lakini ukweli ni kwamba mnanungunika dhidi ya Mungu.”

12. Mose alituma ujumbe kwa Dathani na Abiramu wana wa Eliabu ili waitwe, lakini wao wakasema, “Hatutakuja!

13. Je, ni jambo dogo kwamba umetutoa Misri, nchi inayotiririka maziwa na asali, ili uje kutuua humu jangwani? Tena, unajifanya mkuu wetu!

14. Zaidi ya hayo, hukutuleta kwenye nchi inayotiririka maziwa na asali, wala kutupatia urithi wa mashamba na mashamba ya mizabibu. Unafikiri utawafanya hawa watu kuwa vipofu? Hatutakuja!”

15. Mose alikasirika mno, akamwambia Mwenyezi-Mungu “Usizikubali sadaka za watu hawa. Mimi sijachukua punda wa mtu yeyote, wala sijamdhuru mtu!”

16. Mose akamwambia Kora, “Kesho usikose kuja pamoja na wafuasi wako mbele ya Mwenyezi-Mungu. Aroni pia atakuwapo.

17. Kila mmoja wenu achukue chetezo chake, na kutia ubani, kisha atakipeleka mbele ya Mwenyezi-Mungu; kwa jumla vitakuwa vyetezo 250; wewe pia na Aroni, kila mmoja atakuwa na chetezo chake.”

18. Basi, kila mmoja wao akachukua chetezo chake, akatia makaa ya moto na ubani, kisha wakaenda na kusimama mlangoni mwa hema la mkutano, pamoja na Mose na Aroni.

19. Naye Kora akawakusanya watu wote pamoja, wakasimama mbele ya Mose na Aroni ambao walikuwa mlangoni mwa hema la mkutano. Ndipo utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukawatokea watu wote!

20. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni,

21. “Jitengeni na watu hawa, niwaangamize sasa hivi.”

22. Lakini Mose na Aroni wakajitupa chini kifudifudi na kusema, “Ee Mwenyezi-Mungu uliye asili ya uhai wa binadamu wote. Je, mtu mmoja akikukosea, utaikasirikia jumuiya nzima?”

Kusoma sura kamili Hesabu 16