Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 14:18-32 Biblia Habari Njema (BHN)

18. ‘Mimi Mwenyezi-Mungu si mwepesi wa hasira, ni mwenye fadhili nyingi, na ni mwenye kusamehe uovu na makosa. Lakini kwa vyovyote vile sitakosa kuwaadhibu watoto na wajukuu hadi kizazi cha tatu na cha nne kwa dhambi za wazazi wao.’

19. Nakusihi uwasamehe watu hawa dhambi zao, kadiri ya fadhili zako nyingi kama vile ulivyowasamehe tangu watoke Misri hadi sasa.”

20. Mwenyezi-Mungu akajibu, “Nimewasamehe kama ulivyoomba.

21. Lakini kwa kweli, kama niishivyo na kadiri dunia itakavyojaa utukufu wangu,

22. hakuna hata mmoja wao ambaye amewahi kuuona utukufu wangu na miujiza yangu niliyoifanya Misri na jangwani kisha akazidi kunijaribu mara hizi zote bila ya kutii sauti yangu,

23. ataiona nchi ile niliyoapa kuwapatia babu zao; kadhalika hata wale wanaonidharau pia hawataiona.

24. Bali kwa sababu mtumishi wangu Kalebu ni tofauti, na amenitii kikamilifu, nitamfikisha kwenye nchi hiyo aliyoingia na wazawa wake wataimiliki.

25. Kwa kuwa Waamaleki na Wakanaani wanakaa katika mabonde ya nchi hiyo, kesho geukeni nyuma mwende jangwani kuelekea bahari ya Shamu.”

26. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwuliza Mose na Aroni,

27. “Kundi hili la watu waovu litaendelea kuninungunikia mpaka lini? Nimechoka na haya manunguniko ya Waisraeli juu yangu!

28. Sasa wajibu hivi: Kama niishivyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, nitawatendeeni yaleyale niliyosikia mkiyasema:

29. Mtakufa na miili yenu itatupwa humuhumu jangwani, kwa sababu mmenungunika dhidi yangu, hakuna hata mmoja wenu mwenye umri wa kuanzia miaka ishirini na zaidi,

30. atakayeingia katika nchi hiyo ambayo niliapa kuwapa iwe yenu, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni.

31. Nyinyi mlisema kuwa watoto wenu watatekwa nyara, lakini mimi nitawafikisha watoto wenu kwenye nchi mliyoidharau, ili waijue na iwe makao yao.

32. Lakini nyinyi, mtafia humuhumu jangwani.

Kusoma sura kamili Hesabu 14