Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 10:3-17 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Tarumbeta zote mbili zikipigwa pamoja, watu wote watakusanyika karibu nawe mbele ya lango la hema la mkutano.

4. Lakini kama ikipigwa tarumbeta moja tu, basi ni viongozi tu wa makabila ya Israeli watakaokusanyika karibu nawe.

5. Ishara hiyo ikitolewa kwa kupiga tarumbeta, wakazi wa kambi za mashariki wataanza safari.

6. Ishara hiyo ikipigwa mara ya pili, wale wa kambi za upande wa kusini wataanza kuondoka. Ishara hiyo ya tarumbeta itatolewa kila wakati wa kuanza safari.

7. Lakini wakati wa kuwaita watu wakusanyike pamoja, tarumbeta zitapigwa kwa njia ya kawaida.

8. Wazawa wa Aroni, makuhani, ndio watakaopiga tarumbeta hizo. Utaratibu huo utafuatwa daima katika vizazi vyenu vyote.

9. “Wakati wa vita nchini mwenu dhidi ya adui wanaowashambulia, mtatoa ishara ya vita kwa kupiga tarumbeta hizi ili Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu apate kuwakumbuka na kuwaokoa na adui zenu.

10. Hali kadhalika katika siku zenu za furaha, kama vile sikukuu za mwandamo wa mwezi na sikukuu nyinginezo, mtazipiga tarumbeta hizi wakati mnapotoa sadaka zenu za kuteketezwa na tambiko za sadaka zenu za amani. Hapo mimi Mungu wenu nitawakumbukeni. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”

11. Mnamo siku ya ishirini ya mwezi wa pili, mwaka wa pili tangu wana wa Israeli walipoondoka Misri, wingu lililokuwa juu ya hema la maamuzi liliinuliwa,

12. nao Waisraeli wakaanza safari yao kutoka jangwa la Sinai. Wingu hilo lilipaa na hatimaye likatua katika jangwa la Parani.

13. Kwa mara ya kwanza Waisraeli walifunga safari hiyo kwa amri ya Mwenyezi-Mungu kama ilivyotolewa na Mose.

14. Wale waliokuwa chini ya bendera ya kikosi cha kabila la Yuda, walitangulia, kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Nashoni mwana wa Aminadabu.

15. Nethaneli mwana wa Suari, alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Isakari.

16. Naye Eliabu mwana wa Heloni, alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Zebuluni.

17. Kisha, hema lilishushwa, na watu wa ukoo wa Gershoni na wa Merari ambao walilibeba, walianza kuondoka.

Kusoma sura kamili Hesabu 10