Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 36:26-37 Biblia Habari Njema (BHN)

26. Nitawapeni moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu. Nitauondoa kwenu moyo mgumu kama jiwe na kuwapa moyo wa utii.

27. Nitatia roho yangu ndani yenu; nitawafanya mfuate kanuni zangu na kuzingatia maazimio yangu.

28. Mtakaa katika nchi niliyowapa wazee wenu. Mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.

29. Nitawaokoa kutoka uchafu wenu wote. Nitaiamuru ngano iongezeke, wala sitawaletea njaa tena.

30. Nitayazidisha matunda ya miti na mazao ya mashamba ili msiaibike tena kwa njaa kati ya mataifa.

31. Kisha mtakapokumbuka mienendo yenu miovu na matendo yenu mabaya, mtajichukia wenyewe kwa sababu ya maovu yenu na machukizo mliyofanya.

32. Lakini jueni kwamba sitafanya hivyo kwa ajili yenu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Oneni aibu na kufadhaika kwa sababu ya matendo yenu, enyi Waisraeli!

33. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ile nitakapowasafisheni maovu yenu yote, nitaifanya miji yenu ikaliwe, nayo magofu yajengwe upya.

34. Nchi iliyokuwa jangwa italimwa tena, hata atakayepita huko hataiona kuwa jangwa.

35. Nao watu watasema: ‘Nchi hii iliyokuwa jangwa, sasa imekuwa kama bustani ya Edeni, nayo miji iliyokuwa ukiwa, mahame na magofu, sasa inakaliwa na watu, tena ina ngome!’

36. Hapo mataifa yaliyobaki kandokando yenu, yatatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu niliyejenga upya yaliyoharibiwa na kupanda mbegu katika nchi iliyokuwa jangwa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema, na nitafanya hayo.

37. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Waisraeli wataniomba niwafanye kuwa wengi kama kundi la kondoo, nami nitawafanya hivyo.

Kusoma sura kamili Ezekieli 36