Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 36:21-36 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Hiyo ilinifanya kuhangaika juu ya jina langu takatifu ambalo watu wa Israeli walilikufuru miongoni mwa mataifa walikokwenda.

22. Basi, waambie Waisraeli kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ninachotaka kufanya si kwa faida yenu nyinyi watu wa Israeli, bali ni kwa heshima ya jina langu takatifu mlilolikufuru miongoni mwa mataifa mlikokwenda.

23. Nitalirudishia hadhi yake takatifu jina langu kuu mlilokufuru miongoni mwa mataifa. Hapo ndipo mataifa yatakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitawatumia nyinyi kuonesha utakatifu wangu mbele yao.

24. Nitawaondoa nyinyi katika kila taifa na kuwakusanya kutoka nchi zote za kigeni; nitawarudisha katika nchi yenu wenyewe.

25. Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtatakata uchafu wenu wote na sanamu za miungu yenu yote.

26. Nitawapeni moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu. Nitauondoa kwenu moyo mgumu kama jiwe na kuwapa moyo wa utii.

27. Nitatia roho yangu ndani yenu; nitawafanya mfuate kanuni zangu na kuzingatia maazimio yangu.

28. Mtakaa katika nchi niliyowapa wazee wenu. Mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.

29. Nitawaokoa kutoka uchafu wenu wote. Nitaiamuru ngano iongezeke, wala sitawaletea njaa tena.

30. Nitayazidisha matunda ya miti na mazao ya mashamba ili msiaibike tena kwa njaa kati ya mataifa.

31. Kisha mtakapokumbuka mienendo yenu miovu na matendo yenu mabaya, mtajichukia wenyewe kwa sababu ya maovu yenu na machukizo mliyofanya.

32. Lakini jueni kwamba sitafanya hivyo kwa ajili yenu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Oneni aibu na kufadhaika kwa sababu ya matendo yenu, enyi Waisraeli!

33. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ile nitakapowasafisheni maovu yenu yote, nitaifanya miji yenu ikaliwe, nayo magofu yajengwe upya.

34. Nchi iliyokuwa jangwa italimwa tena, hata atakayepita huko hataiona kuwa jangwa.

35. Nao watu watasema: ‘Nchi hii iliyokuwa jangwa, sasa imekuwa kama bustani ya Edeni, nayo miji iliyokuwa ukiwa, mahame na magofu, sasa inakaliwa na watu, tena ina ngome!’

36. Hapo mataifa yaliyobaki kandokando yenu, yatatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu niliyejenga upya yaliyoharibiwa na kupanda mbegu katika nchi iliyokuwa jangwa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema, na nitafanya hayo.

Kusoma sura kamili Ezekieli 36