Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 36:12-29 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Nitawafanya watu wangu Israeli watembee juu yenu. Nanyi mtakuwa milki yao, wala hamtawafanya tena wafiwe na watoto wao.

13. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa vile watu wamesema juu yenu kwamba mnakula watu, na mmelipokonya taifa lenu watoto wake,

14. basi, sasa hamtakula tena watu wala kupokonya taifa lenu watoto wake. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.

15. Sitaruhusu tena mataifa yawatukane, wala kuwadharau tena. Hamtasababisha taifa lenu likose. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”

16. Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:

17. “Wewe mtu! Waisraeli walipoishi katika nchi yao waliitia unajisi kwa mienendo na matendo yao. Niliyaona matendo yao kuwa sawa na mwanamke aliye najisi wakati wa siku zake.

18. Niliwamwagia ghadhabu yangu kwa sababu ya damu waliyomwaga katika nchi na kwa sababu ya miungu ambayo kwayo nchi ilitiwa unajisi.

19. Niliwatawanya kati ya mataifa, wakasambazwa katika nchi nyingine. Niliwaadhibu kadiri ya tabia yao na matendo yao.

20. Hata walipokuwa miongoni mwa mataifa walilikufuru jina langu takatifu, hata watu wakasema hivi juu yao: ‘Tazama! Hawa ndio wale watu wa Mwenyezi-Mungu, lakini wamelazimika kuondoka katika nchi yake!’

21. Hiyo ilinifanya kuhangaika juu ya jina langu takatifu ambalo watu wa Israeli walilikufuru miongoni mwa mataifa walikokwenda.

22. Basi, waambie Waisraeli kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ninachotaka kufanya si kwa faida yenu nyinyi watu wa Israeli, bali ni kwa heshima ya jina langu takatifu mlilolikufuru miongoni mwa mataifa mlikokwenda.

23. Nitalirudishia hadhi yake takatifu jina langu kuu mlilokufuru miongoni mwa mataifa. Hapo ndipo mataifa yatakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitawatumia nyinyi kuonesha utakatifu wangu mbele yao.

24. Nitawaondoa nyinyi katika kila taifa na kuwakusanya kutoka nchi zote za kigeni; nitawarudisha katika nchi yenu wenyewe.

25. Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtatakata uchafu wenu wote na sanamu za miungu yenu yote.

26. Nitawapeni moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu. Nitauondoa kwenu moyo mgumu kama jiwe na kuwapa moyo wa utii.

27. Nitatia roho yangu ndani yenu; nitawafanya mfuate kanuni zangu na kuzingatia maazimio yangu.

28. Mtakaa katika nchi niliyowapa wazee wenu. Mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.

29. Nitawaokoa kutoka uchafu wenu wote. Nitaiamuru ngano iongezeke, wala sitawaletea njaa tena.

Kusoma sura kamili Ezekieli 36