Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 29:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kumi, mwaka wa kumi tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:

2. “Wewe mtu! Mgeukie Farao mfalme wa Misri, utoe unabii juu yake na nchi yote ya Misri.

3. Mwambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:Mimi nitapambana na wewe mfalme wa Misri,wewe mamba ulalaye mtoni Nili!Wewe unafikiri kwamba Nili ni wako,kwamba wewe ndiwe uliyeufanya!

4. Basi, nitakutia ndoana tayani mwako,na kufanya samaki wakwame magambani mwako.Nitakuvua kutoka huko mtoni.

5. Nitakutupa jangwani,wewe na samaki hao wote.Mwili wako utaanguka mbugani;wala hakuna atakayekuokota akuzike.Nimeutoa mwili wakouwe chakula cha wanyama wakali na ndege.

6. Hapo ndipo wakazi wote wa Misri watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.“Waisraeli walikutegemea wewe ee Misri, lakini umekuwa dhaifu kama utete.

7. Walipokushika kwa mkono, ulivunjika na kutegua mabega yao. Walipokuegemea ulivunjika na kutetemesha viungo vyao.

8. Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitazusha upanga dhidi yako na kuwaua watu na wanyama wako wote.

9. Kwa sababu umesema kuwa mto Nili ni wako, kwamba ndiwe uliyeufanya, basi, nchi yako, Misri, itakuwa tupu na jangwa. Ndipo watu watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.

10. Hakika nitakuadhibu wewe na mito yako; kwa hiyo nitaifanya nchi ya Misri kuwa jangwa na tupu toka Migdoli mpaka Syene hadi mipakani mwa Kushi.

11. Hakuna mtu wala mnyama atakayepita huko. Haitakaliwa kwa muda wa miaka arubaini.

12. Kati ya miji yote iliyoharibiwa, miji ya Misri itakuwa mitupu kwa miaka arubaini. Nitawatawanya Wamisri kati ya watu wa mataifa mengine na kuwasambaza katika nchi nyingine.

Kusoma sura kamili Ezekieli 29