Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 16:36-51 Biblia Habari Njema (BHN)

36. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuambia kwamba, wewe umetapanya fedha, umefunua uchi wako ili kuzini na wapenzi wako, umeziabudu sanamu zako zote za miungu na kuzitolea damu ya watoto wako.

37. Basi, mimi nitawakusanya wapenzi wako wote uliojifurahisha nao, wote uliowapenda na wote uliowachukia. Nitawakusanya toka pande zote wakushambulie. Nitawafunulia uchi wako wapate kuuona.

38. Nitakuhukumu kama wanavyohukumiwa wanawake wanaovunja ahadi ya ndoa au wauaji; nitakuhukumu kwa adhabu ya kifo kwa hasira na kwa ajili ya wivu.

39. Nitakutia mikononi mwa wapenzi wako, nao watabomoa jukwaa lako na mahali pako pa ibada. Watakuvua mavazi yako na kukunyanganya vito vyako, wakuache uchi, bila kitu.

40. Watakuletea jeshi kukushambulia; watakuua kwa kukupiga mawe na kisha watakukatakata kwa mapanga yao.

41. Nyumba zako watazichoma moto na kuwafanya wanawake wengi waone adhabu yako. Utakoma kujitoa kwa mtu yeyote afanye uzinzi nawe.

42. Hivyo, nitaitosheleza ghadhabu yangu juu yako, wivu niliokuwa nao juu yako utakwisha; nitatulia na wala sitaona hasira tena.

43. Wewe umesahau yale ambayo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nilikufanyia ulipokuwa kijana. Wewe umenichukiza mno kwa mambo hayo yote. Basi, nitakulipiza kisasi kuhusu kila kitu ulichotenda. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Je, hukuongeza uchafu juu ya machukizo yako yote?

44. “Ewe Yerusalemu! Mtu akitaka kutumia methali juu yako atasema: ‘Kama mama alivyo ndivyo alivyo binti yake.’

45. Kweli wewe ni mtoto wa mama aliyemchukia mumewe na watoto wake; wewe ni sawa na dada zako waliowachukia waume zao na watoto wao. Mama yako alikuwa Mhiti na baba yako alikuwa Mwamori.

46. Dada yako mkubwa ni Samaria, aliyekaa upande wako wa kaskazini mwako pamoja na binti zake. Dada yako mdogo ni Sodoma, aliyekaa upande wako wa kusini pamoja na binti zake.

47. Lakini wewe hukutosheka kufuata mienendo yao au kutenda sawa na machukizo yao. Kwa muda mfupi tu ulipotoka kuliko walivyopotoka wao katika mienendo yako yote.

48. Kweli naapa kwa nafsi yangu, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu kuwa, dada yako Sodoma na binti zake, hawakufanya maovu kama yale uliyotenda wewe na binti zako.

49. Kosa la dada yako Sodoma, lilikuwa hili: Yeye pamoja na binti zake walipokuwa na chakula na fanaka tele, walianza kujivuna, wakaacha kuwasaidia maskini na fukara.

50. Walijivuna, wakafanya machukizo mbele yangu. Kwa hiyo niliwaangamiza mara tu nilipoyaona hayo.

51. Naye Samaria kwa kweli hakutenda hata nusu ya dhambi zako. Wewe umefanya machukizo mengi kuliko wao. Ukilinganisha maovu yako na ya dada zako, maovu yao si kitu!

Kusoma sura kamili Ezekieli 16