Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 16:14-28 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Sifa zako zikaenea kati ya mataifa kutokana na uzuri wako, kwani uzuri wako ulikamilika kwa sababu ya fahari niliyokujalia. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.

15. “Lakini, ulitegemea uzuri wako, ukatumia sifa yako kwa kufanya uzinzi, ukifanya umalaya na mtu yeyote apitaye.

16. Ulitwaa baadhi ya mavazi yako, ukayatumia kupambia mahali pako pa ibada na hapo ndipo ukafanyia uzinzi wako. Jambo la namna hiyo halijapata kutokea wala halitatokea kamwe!

17. Vito vyako vizuri vya dhahabu na fedha nilivyokupa, ulivitwaa, ukajifanyia sanamu za wanaume upate kufanya uzinzi nazo.

18. Ukatwaa mavazi niliyokupa yaliyotiwa nakshi na kuzifunika zile sanamu, na mafuta yangu na ubani wangu, ukazitolea sanamu hizo.

19. Chakula changu nilichokupa, ulikitoa kwa sanamu hizo kuwa harufu ya kupendeza kwani nilikulisha kwa unga safi, mafuta na asali. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema!

20. “Tena, watoto wako wa kiume na wa kike ulionizalia uliwatwaa, ukazitambikia sanamu zako kwa kuwateketeza. Je, unadhani uzinzi wako ulikuwa ni jambo dogo?

21. Je, jambo hili la kuwachinja watoto wangu ili wawe tambiko ya kuteketeza kwa ajili ya sanamu zako ni jambo dogo?

22. Katika machukizo yako yote pamoja na uzinzi wako hukuzikumbuka siku za utoto wako, wakati ulipokuwa uchi kabisa, bila kitu, ukigaagaa katika damu yako!

23. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuambia: Ole wako, ole wako Yerusalemu! Baada ya kufanya hayo yote

24. ulijijengea majukwaa ya ibada na mahali pa juu kila mahali.

25. Mwanzoni mwa kila barabara ulijijengea mahali pa juu, ukautumia urembo wako kufanya uzinzi ukijitoa kwa kila mpita njia na kuongeza uzinzi wako.

26. Tena ulifanya uzinzi na jirani zako Wamisri waliojaa tamaa, ukaongeza uzinzi wako na kuichochea hasira yangu.

27. Basi, niliunyosha mkono wangu kukuadhibu. Nilipunguza chakula chako, nikakuacha kwa maadui zako, binti za Wafilisti ambao waliona aibu mno juu ya tabia yako chafu mno.

28. “Kwa kuwa hukutosheka, ulifanya tena uzinzi na Waashuru. Na hiyo pia haikukutosheleza.

Kusoma sura kamili Ezekieli 16