Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 11:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Roho ya Mungu ikaninyanyua na kunipeleka mpaka lango la mashariki la nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Huko nikawaona watu ishirini na watano wakiwamo Yaazania mwana wa Azuri na Pelatia mwana wa Benaya, ambao ni viongozi wa Waisraeli.

2. Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Wewe mtu, hawa ndio watu watungao uovu na kutoa mashauri mabaya mjini humu.

3. Wanasema, ‘Wakati wa kujenga nyumba bado. Mji ni kama chungu, na sisi ni kama nyama.’

4. Kwa hiyo, toa unabii dhidi yao! Tabiri ewe mtu!”

5. Kisha roho ya Mwenyezi-Mungu ikanijia, naye akaniambia, “Waambie watu, Mwenyezi-Mungu asema hivi: Naam, hiki ndicho mnachofikiri enyi Waisraeli. Najua mambo mnayofikiria moyoni mwenu.

6. Nyinyi mmewaua watu wengi mjini humu, na kujaza barabara zake na watu waliouawa.

7. “Lakini, mimi, Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Naam, mji huu ni chungu cha kupikia, na wale waliouawa ndio nyama. Nyinyi lazima mtaondolewa mjini.

8. Nyinyi mmeogopa upanga? Basi, mimi nitaleta upanga dhidi yenu!

9. Nitawatoa ndani ya mji na kuwatia mikononi mwa watu wa mataifa mengine, nami nitawahukumu.

10. Mtauawa kwa upanga, nami nitawahukumu mpakani mwa Israeli. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.

11. Mji wa Yerusalemu hautakuwa tena chungu chenu wala nyinyi hamtakuwa nyama ndani yake. Mimi nitawahukumu mpakani mwa Israeli.

12. Nanyi mtatambua kwamba mimi ni Mwenyezi-Mungu ambaye sheria zake hamkuzifuata na maagizo yake hamkutekeleza, bali mmetenda kulingana na maagizo ya mataifa yanayowazunguka.”

13. Nilipokuwa natabiri, Pelatia mwana wa Benaya akafariki. Nami nikaanguka kifudifudi, nikalia kwa sauti kubwa, nikisema, “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, je, utawamaliza kabisa Waisraeli waliobaki?”

14. Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:

15. “Wewe mtu, ndugu zako na wakazi wa Yerusalemu ambao pia ni ndugu zako wanasema juu yako na juu ya watu wote wa Israeli walioko uhamishoni, ‘Nyinyi mlio uhamishoni mko mbali sana na Mwenyezi-Mungu; maana Mwenyezi-Mungu ametupa sisi nchi hii iwe mali yetu.’

16. “Lakini, waambie hao walio uhamishoni kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ingawa nimewapeleka mbali miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi nyingine, hata hivyo, kwa wakati uliopo mimi nipo pamoja nao huko waliko.

17. “Basi, waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawakusanya toka miongoni mwa watu mnakokaa. Nitawakusanya kutoka nchi ambako mlitawanywa. Nitawarudisha nchini Israeli.

Kusoma sura kamili Ezekieli 11