Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 10:9-22 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Niliangalia, nikaona kulikuwa na magurudumu manne, gurudumu moja pembeni mwa kila kiumbe chenye mabawa. Magurudumu hayo yalimetameta kama jiwe la zabarajadi.

10. Yote manne yalionekana kuwa ya namna moja, na kila gurudumu lilionekana kama liko ndani ya gurudumu lingine.

11. Yaliweza kwenda pande zote bila kugeuka; kule lilikoelekea gurudumu la kwanza yote yalifuata.

12. Miili ya hao viumbe, migongo yao, mikono na mabawa yao, pamoja na magurudumu, vyote vilijaa macho pande zote.

13. Niliambiwa kuwa magurudumu yale yanaitwa, “Magurudumu Yanayozunguka.”

14. Kila kiumbe mwenye mabawa alikuwa na nyuso nne: Uso wa kwanza ulikuwa wa fahali, uso wa pili ulikuwa wa mwanadamu, uso wa tatu ulikuwa wa simba na uso wa nne ulikuwa wa tai.

15. Viumbe wenye mabawa wakainuka juu. Hawa ndio wale viumbe hai niliowaona karibu na mto Kebari.

16. Viumbe hao walipokwenda, magurudumu nayo yalikwenda kando yao. Viumbe walipokunjua mabawa yao ili kupaa juu, magurudumu nayo yalikwenda pamoja nao.

17. Waliposimama, magurudumu nayo yalisimama; hao walipopaa juu, magurudumu nayo yalipaa pamoja nao. Roho ya hao viumbe ilikuwa pia katika magurudumu hayo.

18. Kisha utukufu wa Mwenyezi-Mungu ulitoka kwenye kizingiti cha nyumba, ukaenda na kusimama juu ya wale viumbe.

19. Viumbe wakakunjua mabawa yao, wakapaa juu, mimi nikiwa nawaona na yale magurudumu yalikuwa kando yao. Wakasimama mbele ya lango la mashariki la nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao.

20. Hawa walikuwa wale viumbe hai niliowaona chini ya Mungu wa Israeli karibu na mto Kebari, nami nikatambua kuwa ni viumbe wenye mabawa.

21. Kila mmoja wao alikuwa na nyuso nne na mabawa manne; na chini ya kila bawa kulikuwa na kitu kama mkono wa binadamu.

22. Vilevile nilizitambua nyuso zao: Zilikuwa zilezile nilizokuwa nimeziona kule kwenye mto Kebari. Kila kiumbe alikwenda mbele, moja kwa moja.

Kusoma sura kamili Ezekieli 10