Agano la Kale

Agano Jipya

Danieli 7:14-24 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Akapewa mamlaka, utukufu na ufalme, ili watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote wamtumikie. Utawala wake ni wa milele na ufalme wake kamwe hautaangamizwa.

15. “Maono niliyoyaona mimi Danieli yalinishtua, nami nikafadhaika.

16. Nilimkaribia mmojawapo wa wale waliosimama huko na kumwuliza maana halisi ya mambo hayo yote. Naye akanisimulia na kunieleza maana yake:

17. ‘Wanyama hao wanne wakubwa ni wafalme wanne watakaotokea duniani.

18. Lakini watakatifu wa Mungu Mkuu watapewa ufalme, nao wataumiliki ufalme huo milele na milele.’

19. “Kisha nikataka nielezwe juu ya yule mnyama wa nne, ambaye alikuwa tofauti kabisa na wale wengine, wa ajabu na wa kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma na makucha yake ya shaba. Aliyatumia meno hayo kula na kuvunjavunja, na mabaki aliyakanyagakanyaga kwa nyayo zake.

20. Aidha nilitaka nielezwe juu ya zile pembe kumi alizokuwa nazo kichwani mwake, na ule upembe mmoja ambao kabla haujaota, zilingoka pembe tatu; upembe uliokuwa na macho na kinywa ambacho kilitamka maneno ya kujigamba, na ambao ulionekana kuwa mkubwa kuliko pembe nyingine.

21. “Nikiwa bado naangalia, pembe hiyo ilipigana vita na watakatifu, nayo ikawashinda.

22. Lakini yule ‘Mzee wa kale na kale’ akainuka, akawapa haki watakatifu wa Mungu na wakati ulipotimia, hao watakatifu wakapewa ufalme.

23. “Nikaelezwa hivi: ‘Yule mnyama wa nne ni ufalme wa nne utakaokuwako duniani. Ufalme huo utakuwa tofauti na falme nyingine, nao utaiangamiza dunia nzima. Utaibwaga chini na kuipasua vipandevipande.

24. Zile pembe kumi ni wafalme kumi watakaotokana na ufalme huo. Halafu watafuatwa na mfalme mwingine ambaye atakuwa tofauti na wale waliomtangulia, na atawaangusha wafalme watatu.

Kusoma sura kamili Danieli 7