Agano la Kale

Agano Jipya

Danieli 4:23-37 Biblia Habari Njema (BHN)

23. Kisha ukaona tena, ee mfalme, Mlinzi mtakatifu akishuka kutoka mbinguni, akaamuru: ‘Ukateni mti huu, mkauangamize. Lakini acheni kisiki chake na mizizi yake ardhini kwenye majani mabichi ya kondeni, kikiwa kimefungwa hapo kwa mnyororo wa chuma na shaba. Mwacheni mtu huyo aloweshwe kwa umande wa mbinguni; mwacheni aishi pamoja na wanyama wa porini kwa miaka saba.’

24. “Hii basi, bwana wangu, ndiyo maana ya ndoto yako, kadiri ya uamuzi wa Mungu Mkuu juu yako:

25. Wewe utafukuzwa mbali na wanaadamu! Utaishi pamoja na wanyama wa porini, utakula majani kama ng'ombe; utalowa kwa umande wa mbinguni. Utakaa katika hali hiyo kwa miaka saba, na mwishowe utatambua kwamba Mungu Mkuu ndiye mwenye uwezo juu ya falme za wanaadamu, na humpa ufalme mtu yeyote amtakaye.

26. Tena amri ile ya kukiacha kisiki na mizizi ya mti huo ardhini ina maana hii: Wewe utarudishiwa tena ufalme wako hapo utakapotambua kwamba Mungu wa mbinguni ndiye atawalaye.

27. Kwa sababu hiyo, ee mfalme, sikiliza shauri langu. Achana na dhambi zako na maovu yako, utende haki na kuwaonea huruma waliodhulumiwa; huenda muda wako wa fanaka ukarefushwa!”

28. Hayo yote yalimpata mfalme Nebukadneza.

29. Miezi kumi na miwili baadaye, mfalme Nebukadneza alikuwa anatembea juu ya dari ya ikulu ya mji wa Babuloni.

30. Basi, akasema kwa sauti, “Tazama Babuloni, mji mkuu nilioujenga kwa nguvu zangu uwe makao yangu ya kifalme na kwa ajili ya utukufu wangu!”

31. Mara tu alipotamka maneno hayo, sauti kutoka mbinguni ikatamka: “Ewe mfalme Nebukadneza, sikiliza ujumbe huu juu yako! Ufalme umekutoka!

32. Utafukuzwa mbali na wanaadamu! Utaishi pamoja na wanyama wa porini kondeni, na utakula majani kama ng'ombe! Utakaa katika hali hiyo kwa muda wa miaka saba, na mwishowe utatambua kwamba Mungu Mkuu ndiye mwenye uwezo juu ya falme za wanaadamu, na humpa ufalme mtu yeyote amtakaye.”

33. Mara moja jambo hilo juu ya mfalme Nebukadneza likatekelezwa. Alifukuzwa mbali na wanaadamu, akawa anakula majani kama ng'ombe. Alilowa kwa umande wa mbinguni, na nywele zake zikawa ndefu kama manyoya ya tai, na kucha zake kama za ndege.

34. “Mwishoni mwa ile miaka saba, mimi Nebukadneza niliinua macho yangu kutazama juu mbinguni na akili zangu zikanirudia. Nilimshukuru Mungu Mkuu na kumheshimu yeye aishiye milele:Kwa sababu enzi yake ni enzi ya milele,ufalme wake wadumu kizazi hata kizazi.

35. Wakazi wote wa dunia si kitu;hufanya atakavyo na viumbe vya mbinguni,na wakazi wa duniani;hakuna awezaye kumpinga,au kusema ‘Unafanya nini?’

36. “Wakati huo huo akili zangu zikanirudia; nilirudishiwa pia heshima yangu, fahari yangu na utukufu wa ufalme wangu. Washauri na maofisa wangu walikuja kunitafuta, nikarudishwa katika ufalme wangu na kupata heshima kama pale awali.

37. “Na sasa, mimi Nebukadneza ninamsifu na kumtukuza na kumheshimu mfalme wa mbinguni. Maana matendo yake yote ni ya haki, naye huwashusha wenye kiburi.”

Kusoma sura kamili Danieli 4