Agano la Kale

Agano Jipya

Danieli 4:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Mimi mfalme Nebukadneza, nawaandikia watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote kote duniani. Nawatakieni amani tele!

2. Nimeona vema kuwajulisha ishara na maajabu ambayo Mungu Mkuu amenionesha.

3. Jinsi gani zilivyo kubwa ishara zake Mungu!Maajabu yake ni makuu mno!Ufalme wake ni ufalme wa milele;enzi yake yadumu kizazi hata kizazi.

4. “Mimi, Nebukadneza, nilikuwa ninaishi raha mstarehe nyumbani kwangu na kufana katika ikulu yangu.

5. Lakini nikaota ndoto iliyonitisha; nikiwa nimelala kitandani, mawazo na maono kichwani mwangu yaliniogopesha.

6. Hivyo, nikaamuru wenye hekima wote wa Babuloni waletwe mbele yangu ili wanieleze maana ya ndoto hiyo.

7. Ndipo waganga, walozi, Wakaldayo na wanajimu wakaletwa. Nikawasimulia ndoto yangu, lakini hawakuweza kunieleza maana yake.

8. Baadaye, akaja Danieli, anayeitwa pia Belteshaza, jina la mungu wangu, ambaye roho ya miungu mitakatifu imo ndani yake. Nami nikamsimulia ndoto yangu, nikasema:

9. Ee Belteshaza, uliye mkuu wa waganga, nafahamu kuwa roho ya miungu mitakatifu imo ndani yako, na kwamba hakuna fumbo lililo gumu kwako. Hii ndiyo ndoto yangu; niambie maana yake.

10. “Nilipokuwa nimelala, niliona maono haya: Niliona mti mrefu sana katikati ya dunia.

11. Mti uliendelea kukua, ukawa imara na kilele chake kikafika mbinguni. Uliweza kuonekana kutoka kila mahali duniani.

12. Majani yake yalikuwa mazuri. Ulikuwa umejaa matunda, kiasi cha kuitosheleza dunia nzima. Wanyama wote wa porini walipata kivuli chini yake, na ndege wa angani walikaa katika matawi yake. Viumbe vyote vilipata chakula kutoka mti huo.

13. “Nilipokuwa nimelala kitandani, niliona maono: Mlinzi mtakatifu alishuka kutoka mbinguni.

14. Akapaaza sauti akisema, ‘Kateni mti huu na kuyakatakata matawi yake. Pukuteni majani yake na kuyatawanya matunda yake. Wanyama na watoroke chini yake na ndege kutoka matawi yake.

15. Lakini acheni kisiki chake na mizizi yake ardhini, kwenye majani mabichi ya kondeni kikiwa kimefungwa hapo kwa mnyororo wa chuma na shaba. Mwacheni mtu huyo aloweshwe kwa umande wa mbinguni; mwacheni aishi pamoja na wanyama wa porini na kula nyasi mbugani.

16. Akili yake ya utu ibadilishwe, awe na akili ya mnyama kwa miaka saba.

17. Hii ni hukumu iliyotangazwa na walinzi; ni uamuzi wa walio watakatifu, ili wanaadamu wote kila mahali wapate kutambua kuwa Mungu Mkuu anayo mamlaka juu ya falme zote za wanaadamu; yeye humpa ufalme mtu yeyote ampendaye, humfanya mfalme hata mtu duni wa mwisho.’

18. “Hii ndiyo ndoto niliyoota mimi Nebukadneza. Sasa, wewe Belteshaza, nieleze maana yake; kwani wenye hekima wote katika ufalme wangu hawawezi kuniambia maana yake; lakini wewe utaweza kwa kuwa roho ya miungu mitakatifu imo ndani yako.”

19. Hapo, Danieli, aliyeitwa pia Belteshaza, akashangaa kwa muda, na fikira zake zikamfadhaisha. Mfalme akamwambia, “Belteshaza, ndoto hii, wala maana yake visikufadhaishe!” Belteshaza akamjibu, “Bwana wangu, laiti ndoto hii na maana yake ingewahusu adui zako!

20. Mti uliouona ukiwa mkubwa na wenye nguvu, ambao matawi yake marefu yalifika mbinguni, nao ukionekana kutoka kila mahali duniani,

Kusoma sura kamili Danieli 4