Agano la Kale

Agano Jipya

Danieli 2:7-20 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Wao wakamjibu mara ya pili, “Mfalme, tusimulie ndoto hiyo, nasi watumishi wako tutakufasiria.”

8. Hapo mfalme akawakatiza kwa kusema, “Najua kweli kwamba mnajaribu kupoteza wakati kwa kuwa mnaona kwamba nilikwisha toa kauli yangu kamili,

9. kwamba msiponijulisha ndoto hiyo, adhabu yenu ni moja. Mmepatana kunidanganyadanganya na kunilaghailaghai huku muda unapita. Niambieni ndoto hiyo, nami nitajua kuwa mnaweza kunijulisha maana yake.”

10. Wale Wakaldayo wakamjibu: “Mfalme, hakuna mtu yeyote duniani awezaye kutimiza matakwa yako. Hakuna mfalme yeyote, hata awe mkuu na mwenye nguvu kiasi gani aliyepata kuwauliza waganga au walozi au Wakaldayo jambo kama hilo.

11. Jambo unalouliza, ee mfalme, ni gumu. Hakuna mtu anayeweza kukufunulia isipokuwa miungu peke yake ambayo haikai miongoni mwa wanaadamu.”

12. Kusikia hivyo, mfalme Nebukadneza alikasirika na kughadhibika sana, akaamuru wenye hekima wote wa Babuloni waangamizwe.

13. Basi, tangazo likaenea kuwa wenye hekima wote wauawe; Danieli na wenzake, nao pia wakatafutwa ili wauawe.

14. Basi, Danieli, kwa tahadhari na busara, alimwendea Arioko, mkuu wa kikosi cha walinzi wa mfalme na ambaye alipewa jukumu la kuwaua wenye hekima wa Babuloni,

15. akamwuliza, “Kwa nini amri ya mfalme ni kali hivyo?” Hapo Arioko akamsimulia Danieli kisa chote.

16. Ndipo Danieli alipomwendea mfalme na kumwomba ampe muda ili aweze kumjulisha mfalme maana ya ndoto yake.

17. Kisha, Danieli akarudi nyumbani, akawajulisha wenzake Hanania, Mishaeli na Azaria jambo hilo.

18. Aliwaambia wamwombe Mungu wa mbinguni awaonee huruma kuhusu fumbo hilo, ili wao wasiangamie pamoja na wenye hekima wengine wa Babuloni.

19. Ndipo Danieli alipofunuliwa fumbo hilo usiku katika maono. Naye Danieli akamshukuru Mungu wa mbinguni,

20. akasema,“Na litukuzwe milele na milele jina lake Mungu.Hekima na nguvu ni vyake.

Kusoma sura kamili Danieli 2