Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 6:20-26 Biblia Habari Njema (BHN)

20. Mara walipoingia mjini, Elisha akaomba, akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, wafumbue macho ili waone.” Mwenyezi-Mungu akasikia ombi lake, akawafumbua macho. Nao wakajikuta wako katikati ya mji wa Samaria.

21. Mfalme wa Israeli alipowaona Waaramu, alimwuliza Elisha, “Je, baba, niwaue?”

22. Elisha akajibu, “La, usiwaue. Kwani hawa unaotaka kuwaua uliwateka kwa upanga wako na mshale wako? Wape chakula na maji, wale na kunywa kisha uwaache warudi kwa bwana wao.”

23. Mfalme wa Israeli akawafanyia karamu kubwa; walipomaliza kula na kunywa, akawarudisha kwa bwana wao. Toka wakati huo, Waaramu hawakuishambulia tena nchi ya Israeli.

24. Baadaye, mfalme Ben-hadadi wa Aramu akakusanya jeshi lake lote akatoka na kuuzingira mji wa Samaria.

25. Matokeo yake ilikuwa njaa kali katika mji wa Samaria. Kichwa cha punda kiligharimu vipande themanini vya fedha, na gramu 100 za mavi ya njiwa ziligharimu vipande vitano vya fedha.

26. Siku moja mfalme wa Israeli alipokuwa anatembea juu ya ukuta wa mji, alisikia mwanamke mmoja akimwita, “Nisaidie, ee bwana wangu mfalme!”

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 6