Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 4:8-19 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Siku moja Elisha alikwenda Shunemu, ambako alikaa mama mmoja tajiri. Mama huyu akamwalika Elisha kwa chakula, na toka siku hiyo ikawa kawaida Elisha kula chakula kwake kila alipopitia huko.

9. Mama huyo akamwambia mumewe, “Sina shaka kwamba mtu huyu anayefika kwetu kila mara ni mtakatifu wa Mungu.

10. Mbona basi tusimjengee chumba na huko tumwekee kitanda, meza, kiti na taa, ili akitumie kila anapotutembelea?”

11. Siku moja Elisha akaja huko na kuingia chumbani mwake ili apumzike.

12. Akamwuliza mtumishi wake Gehazi, “Mwite huyu mama Mshunami.” Alipomwita alikuja na kusimama mbele yake.

13. Naye Elisha akamwambia Gehazi, “Mwambie, tumeona jinsi alivyotushughulikia; sasa anataka tumtendee jambo gani? Je, angependa aombewe lolote kwa mfalme au kwa jemadari wa jeshi?” Mama Mshunami akamjibu, “Mimi ninaishi miongoni mwa watu wangu.”

14. Elisha akasema, “Tumfanyie nini basi?” Gehazi akamjibu, “Hakika hana mtoto, na mumewe amekuwa mzee.”

15. Elisha akamwambia, “Mwite.” Naye akamwita. Akaja na kusimama mlangoni.

16. Elisha akamwambia “Majira kama haya mwakani, utakapotimia mwaka ujao, wakati kama huu, utakuwa na mtoto mikononi mwako.” Mama akamjibu, “La, Bwana wangu! Wewe ni mtu wa Mungu; usinidanganye mimi mtumishi wako!”

17. Lakini huyo mwanamke akapata mimba na kuzaa mtoto wakati kama huo mwaka uliofuata, kama Elisha alivyokuwa amemwambia.

18. Mtoto huyo alipokua, alitoka siku moja pamoja na baba yake akafuatana na wavunaji,

19. naye akamwambia baba yake, “Ole, kichwa changu! Naumwa na kichwa!” Baba yake akamwambia mtumishi wake mmoja, “Mpeleke kwa mama yake.”

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 4