Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 4:20-35 Biblia Habari Njema (BHN)

20. Alipofikishwa kwa mama yake, alikaa juu ya magoti ya mama yake mpaka adhuhuri, halafu akafa.

21. Mama yake akampeleka na kumlaza kitandani mwa mtu wa Mungu, akaufunga mlango na kuondoka.

22. Akamwita mumewe na kumwambia, “Nipe mtumishi mmoja na punda mmoja, ili nimwendee mara moja yule mtu wa Mungu, kisha nitarudi.”

23. Mumewe akamwuliza, “Mbona unataka kumwona leo? Leo si siku ya mwezi mwandamo wala Sabato?” Akamjibu, “Usijali.”

24. Akatandika punda na kumwambia mtumishi, “Sasa kaza mwendo, wala usipunguze mpaka nitakapokuambia.”

25. Basi, akaondoka, akaenda mpaka mlima Karmeli alipokuwa mtu wa Mungu.Mtu wa Mungu alipomwona akija, akamwambia Gehazi mtumishi wake, “Tazama, namwona Mshunami akija;

26. kimbia mara moja ukakutane naye na kumwambia, ‘Hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto hajambo?’” Naye Mshunami akamjibu “Hatujambo.”

27. Alipofika mlimani kwa mtu wa Mungu akamshika miguu, naye Gehazi akakaribia ili amwondoe; lakini mtu wa Mungu akamwambia, “Mwache, kwani ana uchungu mkali, naye Mwenyezi-Mungu hakunijulisha jambo hilo.”

28. Huyo mama akamwambia, “Bwana wangu, je, si nilikuomba mtoto? Kwani sikukusihi usije ukanipa matumaini ambayo yangenipa huzuni baadaye?”

29. Elisha akamwambia Gehazi, “Chukua fimbo yangu, uondoke mara moja. Usisimame njiani kumwamkia mtu yeyote, na mtu yeyote akikuamkia njiani, usipoteze wakati kurudisha salamu. Nenda moja kwa moja mpaka nyumbani na kuweka fimbo yangu juu ya mtoto.”

30. Mwanamke akamwambia Elisha, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe uishivyo, sitakuacha.” Basi Elisha akaondoka na kufuatana naye.

31. Gehazi akatangulia mbele, na alipofika akaweka fimbo ya Elisha juu ya uso wa mtoto, lakini hakukuonekana dalili yoyote ya uhai. Akarudi na kukutana na Elisha, akamwambia, “Kijana hakufufuka.”

32. Elisha alipofika, akaingia peke yake chumbani na kuona maiti ya kijana kitandani.

33. Basi, akafunga mlango na kumwomba Mwenyezi-Mungu.

34. Ndipo akajilaza juu ya mtoto, mdomo wake juu ya mdomo wa mtoto, na macho yake juu ya macho ya mtoto na mikono yake juu ya mikono ya mtoto. Na alipokuwa amekaa hivyo, mwili wa mtoto ukaanza kupata joto.

35. Elisha akasimama na kutembeatembea chumbani, kisha akarudi na kujilaza tena juu ya mtoto. Mtoto akapiga chafya mara saba, halafu akafungua macho.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 4