Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 4:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wanafunzi wa manabii akamwendea Elisha, akamwambia, “Mtumishi wako, mume wangu amefariki, na kama ujuavyo, alikuwa mcha Mungu, lakini aliyemwia fedha amekuja kuwatwaa wanangu wawili wawe watumwa wake.”

2. Elisha akamwuliza, “Sasa nikusaidieje? Niambie kile ulicho nacho nyumbani.” Mama huyo mjane akamjibu, “Mimi mtumishi wako sina kitu chochote ila chupa ndogo ya mafuta.”

3. Elisha akamwambia, “Nenda kwa jirani zako uazime vyombo vitupu vingi kadiri utakavyopata.

4. Kisha uende, wewe pamoja na wanao, mjifungie ndani ya nyumba, na muanze kujaza mafuta. Kila chombo mnachojaza, kiwekeni kando.”

5. Akaenda na kujifungia ndani ya nyumba na wanawe na kuanza kumimina mafuta ndani ya vyombo.

6. Vilipojaa vyote, akamwambia mwanawe mmojawapo, “Niletee chombo kingine.” Mwanae akamjibu, “Vyote vimejaa!” Hapo mafuta yakakoma kutiririka.

7. Akarudi kwa mtu wa Mungu na kumweleza habari hizo. Naye mtu wa Mungu akamwambia, “Nenda ukauze hayo mafuta na kulipa madeni yako, ndipo wewe na wanao mtaishi kwa kutumia hayo yatakayobaki.”

8. Siku moja Elisha alikwenda Shunemu, ambako alikaa mama mmoja tajiri. Mama huyu akamwalika Elisha kwa chakula, na toka siku hiyo ikawa kawaida Elisha kula chakula kwake kila alipopitia huko.

9. Mama huyo akamwambia mumewe, “Sina shaka kwamba mtu huyu anayefika kwetu kila mara ni mtakatifu wa Mungu.

10. Mbona basi tusimjengee chumba na huko tumwekee kitanda, meza, kiti na taa, ili akitumie kila anapotutembelea?”

11. Siku moja Elisha akaja huko na kuingia chumbani mwake ili apumzike.

12. Akamwuliza mtumishi wake Gehazi, “Mwite huyu mama Mshunami.” Alipomwita alikuja na kusimama mbele yake.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 4