Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 19:6-19 Biblia Habari Njema (BHN)

6. aliwaambia “Mwambieni bwana wenu kwamba Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Usiogope kwa sababu ya maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wameyasema kunikebehi.

7. Tazama nitamfanya mfalme asikie uvumi, halafu atarudi katika nchi yake na huko nitamfanya auawe kwa upanga.’”

8. Kisha yule jemadari mkuu aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru alikuwa ameondoka Lakishi, aliondoka na kumkuta akiushambulia mji wa Libna.

9. Halafu mfalme alipopata habari kwamba Tirhaka mfalme wa Kushi anakuja kupigana naye, alituma wajumbe kwa Hezekia, akisema,

10. “Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda, ‘Usikubali Mungu wako unayemtegemea akudanganye kwa kukuahidi kwamba mji wa Yerusalemu hautatekwa na mfalme wa Ashuru.

11. Wewe umekwisha sikia jinsi wafalme wa Ashuru walivyozitenda nchi nyingine na kuziangamiza kabisa. Je, wadhani wewe utaokoka?

12. Je, miungu ya mataifa iliokoa Gozani, Harani, na Resefu na Waedeni waliokaa Telasari, mataifa ambayo babu zangu waliyaangamiza?

13. Wako wapi wafalme wa Hamathi, Arpadi, Sefarvaimu, Hena na wa Iva?’”

14. Mfalme Hezekia alipokea barua kutoka kwa wajumbe na kuisoma. Kisha akaenda na kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, naye akaiweka mbele yake Mwenyezi-Mungu.

15. Halafu akamwomba Mwenyezi-Mungu akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, unayekaa katika kiti cha enzi juu ya viumbe wenye mabawa, ni wewe tu uliye Mungu, unayetawala falme zote za ulimwengu. Wewe uliumba nchi na mbingu.

16. Ee Mwenyezi-Mungu, fumbua macho uone, tega sikio lako, uyasikie matusi yote ambayo Senakeribu amepeleka kukutukana wewe Mungu uliye hai.

17. Ee Mwenyezi-Mungu, ni kweli kwamba wafalme wa Ashuru wameangamiza mataifa na nchi zao.

18. Walitupa miungu yao motoni kwa sababu haikuwa miungu ya kweli, bali sanamu za miti na mawe zilizochongwa na mikono ya watu.

19. Sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, nakusihi utuokoe makuchani mwa Senakeribu, falme zote za dunia zijue kwamba ni wewe peke yako, ee Mwenyezi-Mungu, uliye Mungu.”

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 19