Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 19:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mfalme Hezekia alipopata habari hizo, alirarua mavazi yake, akavaa gunia akaingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

2. Aliwaamuru Eliakimu, mkuu wa ikulu, Shebna, katibu, na wazee wa makuhani, wamwendee nabii Isaya mwana wa Amozi, wakiwa wamevaa mavazi ya magunia.

3. Nao wakamwambia Isaya, “Hezekia anasema hivi, ‘Leo ni siku ya huzuni, siku ya kukemewa na ya dharau. Sisi tumekuwa kama mama ambaye anataka kujifungua mtoto, lakini hana nguvu ya kumzaa.

4. Inawezekana Mwenyezi-Mungu, Mungu wako alisikia maneno ya jemadari mkuu, ambaye ametumwa na mfalme wa Ashuru, bwana wake, ili kumtukana Mungu aliye hai; naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atakaripia maneno aliyosikia. Kwa hiyo waombee watu waliobaki.’”

5. Basi, hao watumishi wa mfalme Hezekia walipokwisha fika kwa Isaya,

6. aliwaambia “Mwambieni bwana wenu kwamba Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Usiogope kwa sababu ya maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wameyasema kunikebehi.

7. Tazama nitamfanya mfalme asikie uvumi, halafu atarudi katika nchi yake na huko nitamfanya auawe kwa upanga.’”

8. Kisha yule jemadari mkuu aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru alikuwa ameondoka Lakishi, aliondoka na kumkuta akiushambulia mji wa Libna.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 19