Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 10:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Katika mji wa Samaria kulikuwa na wana sabini wa Ahabu. Yehu akaandika barua na kuzituma kwa watawala wa mji, kwa viongozi na kwa walinzi wa wana wa Ahabu. Barua yenyewe ilisema hivi:

2. “Kwa kuwa mnao miongoni mwenu wana wa mfalme, kadhalika mnao farasi na magari, silaha na miji ya ngome,

3. mchagueni na kumtawaza mwenye uwezo zaidi kati ya wana wa mfalme; halafu mpige vita kwa ajili ya ukoo wa mfalme.”

4. Watawala wa Samaria waliogopa sana na kusema, “Tunawezaje kumpiga Yehu hali mfalme Yoramu na mfalme Ahazia hawakuweza?”

5. Kwa hiyo ofisa mkuu wa nyumba ya mfalme na ofisa mkuu wa mji, wakishirikiana na viongozi wengine na walinzi, wakampelekea Yehu ujumbe huu: “Sisi tu watumwa wako, na tuko tayari kufanya lolote unalosema. Lakini hatutamtawaza mtu yeyote kuwa mfalme; fanya unavyoona vyema.”

6. Yehu akawaandikia barua nyingine akiwaambia: “Ikiwa kweli mko tayari kufuata maagizo yangu, leteni hapa Yezreeli vichwa vya wana wa bwana wenu; nivipate kesho wakati kama huu.”Wana sabini wa mfalme Ahabu waliishi kwa viongozi wa Samaria, ambao walikuwa walezi wao.

7. Basi, barua ilipowafikia waliwachukua hao wana wa mfalme na kuwakata wote sabini. Waliweka vichwa vyao vikapuni na kumpelekea Yehu huko Yezreeli.

8. Kisha mtumishi mmoja akamwendea na kusema, “Vichwa vya wana wa mfalme vimekwisha letwa.” Ndipo akaamuru, “Viwekwe chini katika mafungu mawili kwenye lango la mji; halafu viache vikae huko mpaka asubuhi.”

9. Asubuhi yake akatoka, akasimama na kuwaambia watu wote, “Nyinyi ni waadilifu, angalia mimi nilikula njama dhidi ya bwana wangu na kumuua. Lakini ni nani aliyewaua hawa wote?

10. Jueni ya kwamba maneno yote aliyosema Mwenyezi-Mungu kuhusu jamaa ya Ahabu yametimia. Mwenyezi-Mungu ameyafanya hayo aliyosema kwa njia ya mtumishi wake Elia.”

11. Ndipo Yehu akaua jamaa yote ya Ahabu iliyokuwa inakaa Yezreeli, pamoja na maofisa wake na marafiki na makuhani wake; hakumwacha mtu yeyote.

12. Baadaye Yehu aliondoka Yezreeli, akaelekea Samaria. Akiwa njiani mahali panapoitwa “Kambi ya Wachungaji,”

13. alikutana na jamaa za marehemu Ahazia mfalme wa Yuda akawauliza, “Nyinyi ni kina nani?” Wakamjibu, “Sisi ni jamaa za Ahazia. Tumeteremka huku kuwatembelea wana wa mfalme na wana wa malkia.”

14. Kisha akasema, “Wakamateni wakiwa hai.” Wakawakamata watu arubaini na wawili, wakawaulia karibu na kisima cha “Kambi ya Wachungaji.” Hakuna aliyebaki hata mmoja.

15. Yehu akatoka tena na alipofika njiani akakutana na Yehonadabu mwana wa Rekabu; Yehu akamsalimu, kisha akamwambia “Wewe una mawazo sawa na yangu? Je, utajiunga nami na kunisaidia?” Yehonadabu akamjibu, “Naam, nitajiunga nawe:”Yehu akasema, “Basi, nipe mkono wako.” Wakashikana mikono na Yehu akampandisha garini mwake.

16. Akamwambia, “Fuatana nami ili ujionee jinsi nilivyo mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu.” Basi, wakasafiri pamoja garini mwake.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 10