Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 18:18-31 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Absalomu, wakati wa uhai wake, alikuwa amejijengea na kujisimikia nguzo iliyoko kwenye Bonde la Mfalme, kwani alisema, “Mimi sina mtoto wa kiume wa kudumisha jina langu ili nikumbukwe.” Nguzo hiyo aliipa jina lake, na inaitwa “Nguzo ya Absalomu” mpaka leo.

19. Kisha, Ahimaasi mwana wa Sadoki, akasema, “Niruhusu nikimbie kumpelekea mfalme habari hizi kuwa Mwenyezi-Mungu amemkomboa katika nguvu za adui zake.”

20. Yoabu akamwambia, “Leo, hutapeleka habari hizo. Unaweza kupeleka habari hizo siku nyingine. Lakini leo hutapeleka habari zozote kwa kuwa mwana wa mfalme amekufa.”

21. Ndipo Yoabu akamwambia mtu mmoja, Mkushi, “Wewe, nenda ukamweleze mfalme yale uliyoona.” Mkushi akainama kwa heshima mbele ya Yoabu, akaondoka mbio.

22. Kisha Ahimaasi mwana wa Sadoki akamwambia Yoabu tena, “Haidhuru; niruhusu na mimi nimkimbilie yule Mkushi!” Yoabu akamwambia, “Mbona unataka kukimbia mwanangu? Wewe hutatuzwa lolote kwa habari hizi!”

23. Ahimaasi akamwambia, “Haidhuru; nitakimbia.” Basi, Yoabu akamwambia, “Haya, kimbia.” Kisha Ahimaasi akakimbia akifuata njia ya nyikani akawahi kumpita yule Mkushi.

24. Daudi alikuwa ameketi kati ya malango mawili ya mji. Naye mlinzi wa lango akapanda ukutani hadi juu ya lango na alipoinua macho yake aliona mtu anakimbia peke yake.

25. Huyo mlinzi akapaza sauti akamwambia mfalme. Mfalme akasema, “Kama yuko peke yake, lazima ana habari.” Yule mtu akazidi kukaribia.

26. Mlinzi akamwona mtu mwingine anakimbia, akaita tena langoni akisema, “Tazama, mtu mwingine anakimbia peke yake!” Mfalme akasema, “Naye analeta habari.”

27. Yule mlinzi akasema, “Naona kuwa yule anayekimbia zaidi ni Ahimaasi mwana wa Sadoki.” Mfalme akasema, “Huyo ni mtu mwema, anatuletea habari njema.”

28. Ndipo Ahimaasi akamwambia mfalme kwa sauti kubwa, “Mambo yote ni sawa.” Akainama mbele ya mfalme, akasujudu na kusema, “Na atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ambaye amekukomboa kutoka watu walioinua mikono yao dhidi yako, bwana wangu mfalme.”

29. Mfalme akamwambia, “Je, kijana Absalomu hajambo?” Ahimaasi akasema, “Wakati Yoabu aliponituma mimi mtumishi wako, niliona kulikuwa na kelele nyingi, lakini sikufahamu maana yake.”

30. Mfalme akasema, “Kaa kando, na usimame hapo.” Basi, Ahimaasi akaenda kando na kusimama kimya.

31. Ndipo na yule Mkushi akafika; naye akasema, “Kuna habari njema kwako bwana wangu mfalme! Maana Mwenyezi-Mungu leo hii amekukomboa kutoka nguvu za wale wote walioinuka dhidi yako.”

Kusoma sura kamili 2 Samueli 18