Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 18:13-25 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Kwa upande mwingine, kama ningemtendea kwa hila (na hakuna lolote linalofichika kwa mfalme) wewe mwenyewe ungeniruka.”

14. Yoabu akamwambia, “Mimi sina wakati wa kupoteza pamoja nawe.” Hapo Yoabu akachukua mikuki midogo mitatu mkononi mwake, akaenda na kumchoma Absalomu moyoni, Absalomu akiwa bado hai kwenye tawi la mwaloni.

15. Kisha, vijana kumi waliombebea silaha Yoabu, wakaja kumzunguka Absalomu, wakampiga na kumwua.

16. Ndipo Yoabu akapiga tarumbeta na wanajeshi wote wakarudi kuwafuatia watu wa Israeli, kwani Yoabu aliwakataza.

17. Wakamchukua Absalomu wakamtupa kwenye shimo kubwa msituni na kurundika rundo kubwa sana la mawe. Watu wote wa Israeli wakakimbia, kila mmoja nyumbani kwake.

18. Absalomu, wakati wa uhai wake, alikuwa amejijengea na kujisimikia nguzo iliyoko kwenye Bonde la Mfalme, kwani alisema, “Mimi sina mtoto wa kiume wa kudumisha jina langu ili nikumbukwe.” Nguzo hiyo aliipa jina lake, na inaitwa “Nguzo ya Absalomu” mpaka leo.

19. Kisha, Ahimaasi mwana wa Sadoki, akasema, “Niruhusu nikimbie kumpelekea mfalme habari hizi kuwa Mwenyezi-Mungu amemkomboa katika nguvu za adui zake.”

20. Yoabu akamwambia, “Leo, hutapeleka habari hizo. Unaweza kupeleka habari hizo siku nyingine. Lakini leo hutapeleka habari zozote kwa kuwa mwana wa mfalme amekufa.”

21. Ndipo Yoabu akamwambia mtu mmoja, Mkushi, “Wewe, nenda ukamweleze mfalme yale uliyoona.” Mkushi akainama kwa heshima mbele ya Yoabu, akaondoka mbio.

22. Kisha Ahimaasi mwana wa Sadoki akamwambia Yoabu tena, “Haidhuru; niruhusu na mimi nimkimbilie yule Mkushi!” Yoabu akamwambia, “Mbona unataka kukimbia mwanangu? Wewe hutatuzwa lolote kwa habari hizi!”

23. Ahimaasi akamwambia, “Haidhuru; nitakimbia.” Basi, Yoabu akamwambia, “Haya, kimbia.” Kisha Ahimaasi akakimbia akifuata njia ya nyikani akawahi kumpita yule Mkushi.

24. Daudi alikuwa ameketi kati ya malango mawili ya mji. Naye mlinzi wa lango akapanda ukutani hadi juu ya lango na alipoinua macho yake aliona mtu anakimbia peke yake.

25. Huyo mlinzi akapaza sauti akamwambia mfalme. Mfalme akasema, “Kama yuko peke yake, lazima ana habari.” Yule mtu akazidi kukaribia.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 18