Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 14:21-30 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Kisha, mfalme akamwambia Yoabu, “Sasa sikiliza, natoa kibali changu ili umrudishe nyumbani yule kijana Absalomu.”

22. Yoabu alianguka chini kifudifudi, akasujudu na kumtakia mfalme baraka, akasema, “Leo, mimi mtumishi wako, bwana wangu mfalme, ninajua kuwa nimepata kibali mbele yako, kwa kulikubali ombi langu.”

23. Hivyo, Yoabu aliondoka, akaenda Geshuri kumleta Absalomu mjini Yerusalemu.

24. Lakini mfalme akasema, “Absalomu aishi mbali nami; aishi nyumbani kwake. Asije hapa kuniona.” Hivyo, Absalomu akawa anaishi mbali, nyumbani kwake na hakumwona mfalme Daudi.

25. Katika Israeli yote, hakuna yeyote aliyesifiwa kwa uzuri kama Absalomu. Tangu nyayo zake hadi utosini mwake, Absalomu hakuwa na kasoro yoyote.

26. Kila alipokata nywele zake, (na kila mwishoni mwa mwaka alikata nywele zake kwani zilikuwa nzito), alipozipima, zilikuwa na uzito wa kilo mbili kulingana na vipimo vya kifalme.

27. Absalomu alizaa watoto watatu wa kiume pamoja na binti mmoja jina lake Tamari. Tamari alikuwa mwanamke mzuri.

28. Basi, Absalomu aliishi mjini Yerusalemu kwa muda wa miaka miwili mizima bila kumwona mfalme Daudi.

29. Kisha, Absalomu alimtumia ujumbe Yoabu, ili aende kwa mfalme kwa niaba yake, lakini Yoabu akakataa. Absalomu akatuma ujumbe mara ya pili lakini Yoabu akakataa.

30. Basi, Absalomu akawaambia watumishi wake, “Angalieni Yoabu ana shamba la shayiri karibu na langu. Nendeni mkalichome moto.” Kwa hiyo watumishi wa Absalomu wakalichoma moto shamba la Yoabu.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 14