Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 12:7-16 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Sasa, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: ‘Mimi nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli na kukuokoa mikononi mwa Shauli.

8. Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake zake wawe wako, tena nikakupa watu wa Israeli na wa Yuda uwatawale. Na kama haya yangekuwa kidogo mno kwako ningekuongezea mara mbili zaidi ya hayo.

9. Kwa nini basi, umedharau neno langu mimi Mwenyezi-Mungu ukafanya uovu huu mbele yangu? Umemuua Uria Mhiti, kwa upanga, ukamchukua mke wake kuwa mkeo. Umewatumia Waamoni kumwua Uria vitani!

10. Kwa hiyo basi, kwa kuwa umenidharau na umemchukua mke wa Uria Mhiti, kuwa mkeo, mauaji hayataondoka katika jamaa yako’.

11. Sikiliza, Mwenyezi-Mungu asema, ‘Tazama, nitazusha maafa katika jamaa yako mwenyewe. Nitawachukua wake zako ukiona kwa macho yako mwenyewe na kumpa jirani yako, naye atalala nao hadharani.

12. Wewe ulifanya jambo hilo kwa siri, lakini mimi nitayafanya haya mbele ya Waisraeli wote hadharani.’”

13. Basi, Daudi akamwambia Nathani, “Nimetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu.” Nathani akamwambia, “Mwenyezi-Mungu amekusamehe dhambi yako, nawe hutakufa.

14. Hata hivyo, kwa kuwa kwa tendo lako umemdharau kabisa Mwenyezi-Mungu, mtoto wako atakufa.”

15. Kisha Nathani akarudi nyumbani kwake.Mwenyezi-Mungu alimpiga mtoto ambaye Bathsheba mkewe Uria alimzalia Daudi, naye akawa mgonjwa.

16. Daudi alimwomba Mungu mtoto apate nafuu. Alikwenda chumbani kwake, na usiku kucha akalala sakafuni.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 12