Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 12:21-31 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Ndipo watumishi wake wakamwuliza, “Ni jambo gani hili ulilofanya? Mtoto alipokuwa hai, wewe ulifunga na kumlilia. Lakini alipokufa, umeinuka, ukala chakula.”

22. Daudi akawajibu, “Ni kweli mtoto alipokuwa hai, nilifunga na kulia. Nilifanya hivyo kwani nilifikiri, ‘Nani anajua? Huenda Mwenyezi-Mungu akanirehemu ili mtoto aishi’.

23. Lakini sasa amekufa, ya nini nifunge? Je, mimi naweza kumrudisha duniani? Siku moja, nitakwenda huko alikokwenda, lakini yeye hawezi kurudi kwangu.”

24. Halafu Daudi akamfariji Bathsheba mkewe. Akalala naye, naye akapata mimba na kujifungua mtoto wa kiume, ambaye Daudi alimwita Solomoni. Mwenyezi-Mungu alimpenda mtoto huyo,

25. naye akamtuma nabii Nathani kwa Daudi kuwa amwite mtoto huyo Yedidia kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu.

26. Wakati huo, Yoabu aliushambulia Raba mji wa Waamoni, naye akauteka huo mji wa kifalme.

27. Yoabu akatuma ujumbe kwa Daudi, “Nimeushambulia mji wa Raba, nami nimelikamata bwawa lao la maji.

28. Sasa wakusanye watu wote waliosalia, upige kambi kuuzunguka na kuuteka. La sivyo, nikiuteka, utaitwa kwa jina langu.”

29. Hivyo, Daudi akakusanya watu wote akaenda Raba, akaushambulia na kuuteka mji huo.

30. Kisha akachukua taji ya mfalme wao kutoka kichwani pake. Uzito wa taji hiyo ya dhahabu ulikuwa kilo thelathini na tano; na ndani yake mlikuwamo jiwe la thamani. Naye Daudi akavikwa taji hiyo kichwani pake. Pia aliteka idadi kubwa sana ya nyara katika mji huo.

31. Halafu aliwachukua watu wa mji huo, akawaweka wafanye kazi wakitumia misumeno, sururu za chuma, mashoka ya chuma na kuwatumia kufanya kazi katika tanuri ya matofali; hivyo ndivyo alivyoitenda miji yote ya Waamoni. Hatimaye Daudi na watu wote walirudi Yerusalemu.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 12