Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 12:10-23 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Kwa hiyo basi, kwa kuwa umenidharau na umemchukua mke wa Uria Mhiti, kuwa mkeo, mauaji hayataondoka katika jamaa yako’.

11. Sikiliza, Mwenyezi-Mungu asema, ‘Tazama, nitazusha maafa katika jamaa yako mwenyewe. Nitawachukua wake zako ukiona kwa macho yako mwenyewe na kumpa jirani yako, naye atalala nao hadharani.

12. Wewe ulifanya jambo hilo kwa siri, lakini mimi nitayafanya haya mbele ya Waisraeli wote hadharani.’”

13. Basi, Daudi akamwambia Nathani, “Nimetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu.” Nathani akamwambia, “Mwenyezi-Mungu amekusamehe dhambi yako, nawe hutakufa.

14. Hata hivyo, kwa kuwa kwa tendo lako umemdharau kabisa Mwenyezi-Mungu, mtoto wako atakufa.”

15. Kisha Nathani akarudi nyumbani kwake.Mwenyezi-Mungu alimpiga mtoto ambaye Bathsheba mkewe Uria alimzalia Daudi, naye akawa mgonjwa.

16. Daudi alimwomba Mungu mtoto apate nafuu. Alikwenda chumbani kwake, na usiku kucha akalala sakafuni.

17. Wazee waliokuwa wanamwangalia katika jumba hilo walimfuata na kumsihi aamke, lakini yeye alikataa, na hakula chakula chochote pamoja nao.

18. Juma moja baadaye, mtoto huyo akafa. Watumishi wa Daudi waliogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwani walifikiri, “Mtoto huyo alipokuwa hai, tulizungumza naye, lakini hakutusikiliza. Sasa, tutamwambiaje kuwa mtoto wake amekufa? Huenda akajidhuru.”

19. Daudi alipowaona watumishi wake wananongonezana, akagundua kuwa mtoto wake amekufa. Hivyo, akawauliza, “Je, mtoto amekufa?” Nao wakamjibu, “Naam! Amekufa.”

20. Kisha, Daudi aliinuka kutoka sakafuni, akaoga, akajipaka mafuta na kubadilisha mavazi yake. Halafu akaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuabudu. Kisha akarudi nyumbani na alipotaka chakula, akapewa, naye akala.

21. Ndipo watumishi wake wakamwuliza, “Ni jambo gani hili ulilofanya? Mtoto alipokuwa hai, wewe ulifunga na kumlilia. Lakini alipokufa, umeinuka, ukala chakula.”

22. Daudi akawajibu, “Ni kweli mtoto alipokuwa hai, nilifunga na kulia. Nilifanya hivyo kwani nilifikiri, ‘Nani anajua? Huenda Mwenyezi-Mungu akanirehemu ili mtoto aishi’.

23. Lakini sasa amekufa, ya nini nifunge? Je, mimi naweza kumrudisha duniani? Siku moja, nitakwenda huko alikokwenda, lakini yeye hawezi kurudi kwangu.”

Kusoma sura kamili 2 Samueli 12