Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 35:13-20 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Walimchoma mwanakondoo wa Pasaka juu ya moto kama ilivyoagizwa, na pia walizitokosa sadaka takatifu katika vyungu, masufuria na kwenye vikaango, na kuwagawia upesiupesi watu wasiofanya kazi ya ukuhani.

14. Baadaye, Walawi wakajiandalia sehemu zao na za makuhani kwa maana makuhani wa uzao wa Aroni walikuwa wanashughulika na utoaji wa sadaka za kuteketeza, na vipande vya mafuta, mpaka usiku; kwa hiyo Walawi waliandaa kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya makuhani wa uzao wa Aroni.

15. Nao waimbaji wazawa wa Asafu walishika nafasi zao, kwa mujibu wa maagizo ya mfalme Daudi, Asafu, Hemani na Yeduthuni, mwonaji wa mfalme. Nao mabawabu walikuwa kwenye malango; hawakuhitajika kuziacha nafasi zao za kazi kwa kuwa ndugu zao Walawi waliwaandalia Pasaka.

16. Hivyo basi, huduma yote ya Mwenyezi-Mungu ilitayarishwa siku hiyo, ili kuiadhimisha Pasaka na kutoa sadaka za kuteketeza kwenye madhabahu ya Mwenyezi-Mungu kama alivyoamuru mfalme Yosia.

17. Wakati huo watu wote wa Israeli waliohudhuria waliiadhimisha sikukuu hiyo ya Pasaka na sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, kwa muda wa siku saba.

18. Pasaka kama hiyo ilikuwa haijasherehekewa katika Israeli yote tangu siku za nabii Samueli. Hapajatokea mfalme hata mmoja wa Israeli aliyeadhimisha Pasaka kama hii iliyoadhimishwa na mfalme Yosia pamoja na makuhani, Walawi na watu wote wa Yuda, watu wa Israeli na wakazi wa Yerusalemu.

19. Pasaka hiyo iliadhimishwa katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake mfalme Yosia.

20. Baada ya haya yote aliyofanya mfalme Yosia kwa ajili ya hekalu, Neko, mfalme wa Misri, aliongoza jeshi lake kwenda kushambulia Karkemishi kwenye mto Eufrate. Naye mfalme Yosia alitoka kumkabili,

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 35