Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 33:16-25 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Alirudisha madhabahu ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, na juu yake akatoa tambiko za amani na za shukrani, akawaamuru watu wa Yuda wamwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

17. Hata hivyo watu waliendelea kutoa sadaka mahali pa kufanyia ibada, lakini kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wao tu.

18. Matendo mengine ya Manase, sala yake kwa Mungu wake na maneno ya waonaji waliozungumza naye kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hayo, yote yameandikwa katika Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.

19. Nalo ombi lake na jinsi Mungu alivyompokea, dhambi zake zote na ukosefu wa uaminifu wake, mahali alipojenga pa kuabudia na jinsi alivyotengeneza Ashera na sanamu kabla ya kujinyenyekesha, hayo yameandikwa katika Kumbukumbu za Waonaji.

20. Manase alifariki na kuzikwa katika ikulu yake, naye Amoni, mwanawe, akatawala mahali pake.

21. Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala Yuda; alitawala miaka miwili huko Yerusalemu.

22. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama vile Manase baba yake alivyofanya. Pia alitoa sadaka na kutumikia sanamu ambazo Manase baba yake alichonga.

23. Naye hakujinyenyekesha mbele za Mwenyezi-Mungu, kama alivyofanya Manase, lakini yeye aliongeza kutenda makosa zaidi.

24. Baadaye watumishi wake walikula njama na kumuua katika ikulu yake.

25. Lakini watu wa Yuda wakawaua hao wote waliokula njama dhidi ya Amoni; kisha wakamfanya Yosia, mwanawe kuwa mfalme badala yake.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 33