Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 32:14-21 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Ni mungu gani kati ya miungu ya mataifa hayo iliyoharibiwa kabisa na babu zangu aliyeweza kuwakomboa watu wake kutoka mikononi mwangu ndio nanyi muwe na tumaini ya kwamba Mungu wenu atawaokoeni mikononi mwangu?

15. Msidanganywe na Hezekia wala msishawishike kwa hayo. Msimwamini mtu huyu, kwa maana hapajatokea mungu wa taifa au mfalme yeyote aliyefaulu kuwakomboa watu wake kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru, sembuse huyu Mungu wenu!”

16. Watumishi wa mfalme wa Ashuru walisema maneno mengine mengi mabaya dhidi ya Mwenyezi-Mungu, na dhidi ya Hezekia mtumishi wake.

17. Mfalme mwenyewe aliandika barua akamtukana na kumdharau Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akisema, “Kama vile ambavyo miungu ya mataifa mengine haikuweza kuwaokoa watu wao kutoka mikononi mwangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hataweza kuwaokoa watu wake.”

18. Maofisa hao waliwaambia kwa sauti kubwa kwa lugha ya Kiebrania watu wa Yerusalemu waliokuwa ukutani, wakikusudia kuwatia hofu na woga ili wauteke mji kwa urahisi.

19. Wakazungumza juu ya Mungu wa Yerusalemu kana kwamba ni miungu ya mataifa mengine; sanamu tu zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu!

20. Hapo mfalme Hezekia na nabii Isaya, mwana wa Amozi, wakamwomba Mungu na kumlilia awasaidie kwa ajili ya mambo haya.

21. Naye Mwenyezi-Mungu akatuma malaika, akaenda na kuwakatilia mbali mashujaa, wanajeshi, makamanda na maofisa katika kambi ya mfalme wa Ashuru. Basi, mfalme wa Ashuru akarejea nchini mwake amejawa aibu. Mara alipoingia ndani ya nyumba ya mungu wake, baadhi ya wanawe mwenyewe wakamuua papo hapo kwa upanga.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 32