Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 31:7-18 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Katika mwezi wa tatu walianza kuvipanga katika mafungu, wakamaliza mnamo mwezi wa saba.

8. Mfalme Hezekia na maofisa wake walipokuja kuyaona mafungu hayo, walimtukuza Mwenyezi-Mungu na watu wake wa Israeli.

9. Mfalme Hezekia aliwauliza makuhani na Walawi kuhusu mafungu hayo.

10. Azaria, kuhani mkuu aliyekuwa wa uzao wa Sadoki akamjibu, “Tangu watu waanze kuleta matoleo yao hekaluni, tumekuwa na vyakula vya kutosha na hata tunayo akiba kubwa. Mwenyezi-Mungu amewabariki watu wake, ndiyo maana tumepata vitu hivi vyote.”

11. Kisha mfalme Hezekia akawaamuru watengeneze ghala katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Wakatengeneza;

12. na humo wakaweka matoleo, zaka na vyote vilivyowekwa wakfu, kwa uaminifu. Wakamweka Konania, Mlawi, awe ofisa mkuu mtunzaji wa vitu hivyo, na Shimei nduguye, awe msaidizi wake.

13. Nao Yehieli, Azazia, Nahathi, Asaheli, Yeremothi, Yozabadi, Elieli, Ismakia, Mahathi na Benaya, waliwekwa wawe wasimamizi chini ya uongozi wa Konania na Shimei nduguye. Hawa wote walichaguliwa na mfalme Hezekia na Azaria, ofisa mkuu wa nyumba ya Mungu.

14. Kore mwana wa Imna, Mlawi, aliyekuwa bawabu wa Lango la Mashariki la hekalu, alisimamia matoleo yote ya hiari kwa Mungu, na ugawaji wa matoleo kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na sadaka zilizo takatifu kabisa.

15. Nao Edeni, Miniamini, Yeshua, Shemaya, Amaria na Shekania, walimsaidia kufanya kazi hiyo kwa uaminifu katika ile miji mingine walimoishi makuhani. Waliwagawia ndugu zao Walawi vyakula, wakubwa kwa wadogo.

16. Tena, bila kujali koo walimoandikishwa, waliwapa sehemu wale watoto wa kiume waliokuwa wametimiza umri wa miaka mitatu na zaidi, na ambao waliingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kila siku kutekeleza wajibu wao. Kila mmoja wao alipata sehemu yake kulingana na huduma aliyotoa kwa zamu yake.

17. Makuhani waliandikishwa kulingana na jamaa zao, hali Walawi waliotimiza miaka ishirini na zaidi waliandikishwa kulingana na kazi zao na zamu zao.

18. Waliandikishwa wote pamoja na watoto wao wadogo, wake zao, wana wao na binti zao kwa kuwa, kwa mujibu wa kazi zao, walihitajika kujiweka katika hali ya utakaso kila mara.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 31