Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 31:5-14 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Mara tu amri hii ilipotolewa, watu wa Israeli walitoa kwa wingi, malimbuko ya nafaka, divai, mafuta, asali na mazao mengine mbalimbali ya shambani, na pia zaka nyingi za kila kitu.

6. Watu wa Israeli na Yuda walioishi katika miji ya Yuda, pia wakaleta zaka zao za ng'ombe na kondoo na vitu vingine, wakaviweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Waliviweka vitu hivyo katika mafungu.

7. Katika mwezi wa tatu walianza kuvipanga katika mafungu, wakamaliza mnamo mwezi wa saba.

8. Mfalme Hezekia na maofisa wake walipokuja kuyaona mafungu hayo, walimtukuza Mwenyezi-Mungu na watu wake wa Israeli.

9. Mfalme Hezekia aliwauliza makuhani na Walawi kuhusu mafungu hayo.

10. Azaria, kuhani mkuu aliyekuwa wa uzao wa Sadoki akamjibu, “Tangu watu waanze kuleta matoleo yao hekaluni, tumekuwa na vyakula vya kutosha na hata tunayo akiba kubwa. Mwenyezi-Mungu amewabariki watu wake, ndiyo maana tumepata vitu hivi vyote.”

11. Kisha mfalme Hezekia akawaamuru watengeneze ghala katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Wakatengeneza;

12. na humo wakaweka matoleo, zaka na vyote vilivyowekwa wakfu, kwa uaminifu. Wakamweka Konania, Mlawi, awe ofisa mkuu mtunzaji wa vitu hivyo, na Shimei nduguye, awe msaidizi wake.

13. Nao Yehieli, Azazia, Nahathi, Asaheli, Yeremothi, Yozabadi, Elieli, Ismakia, Mahathi na Benaya, waliwekwa wawe wasimamizi chini ya uongozi wa Konania na Shimei nduguye. Hawa wote walichaguliwa na mfalme Hezekia na Azaria, ofisa mkuu wa nyumba ya Mungu.

14. Kore mwana wa Imna, Mlawi, aliyekuwa bawabu wa Lango la Mashariki la hekalu, alisimamia matoleo yote ya hiari kwa Mungu, na ugawaji wa matoleo kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na sadaka zilizo takatifu kabisa.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 31