Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 30:13-27 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Watu wengi sana walijumuika mjini Yerusalemu mnamo mwezi wa pili, kuiadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu.

14. Walianza kazi, wakaziondoa madhabahu zote zilizokuwa Yerusalemu, na nyingine zote zilizotumiwa kufukizia ubani, wakazibeba na kuzitupa katika Bonde la Kidroni.

15. Siku ya kumi na nne ya mwezi huo walichinja mwanakondoo wa Pasaka. Makuhani na Walawi waliona aibu, wakajitakasa na kuleta sadaka za kuteketeza katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

16. Walichukua nafasi zao hekaluni kulingana na maagizo yaliyokuwamo katika sheria za Mose, mtu wa Mungu. Walawi waliwapa makuhani damu ya tambiko, nao wakainyunyiza madhabahuni.

17. Kwa vile wengi wa wale waliokusanyika hapo hawakuwa wamejitakasa, iliwabidi Walawi kuwachinjia wanakondoo wa Pasaka na kuwaweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu.

18. Aidha miongoni mwa kusanyiko hilo la watu, wengi wa wale waliotoka Efraimu, Manase, Isakari na Zebuluni, walikuwa wakiiadhimisha Pasaka kinyume cha maagizo. Hii ni kwa kuwa mfalme Hezekia aliwaombea akisema, “Mwenyezi-Mungu uliye mwema, msamehe yeyote yule

19. atakayekuomba kwa moyo wake wote wewe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zake, hata ingawa si msafi kulingana na sheria za utakaso.”

20. Mwenyezi-Mungu alikubali ombi la Hezekia, akawasamehe watu hao.

21. Waisraeli wote waliokuwa wamekusanyika mjini Yerusalemu waliiadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu kwa muda wa siku saba, wakiwa na furaha kubwa. Walawi na makuhani walimsifu Mwenyezi-Mungu kila siku, walimwimbia kwa nguvu zao zote.

22. Mfalme Hezekia aliwasifu na kuwatia moyo makuhani kwa kuwa waliendesha ibada kwa ujuzi mwingi.Baada ya kumaliza siku saba wakati ambao watu walikula, wakatoa sadaka za amani na kumtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao,

23. watu waliamua kwa kauli moja kuziendeleza sherehe kwa muda wa siku saba zaidi. Basi, wakaendelea kusherehekea kwa furaha kuu kwa muda wa siku saba zaidi.

24. Mfalme Hezekia wa Yuda aliwapa watu waliokusanyika jumla ya mafahali 1,000 na kondoo 7,000. Hali kadhalika, wakuu wakawapa mafahali 1,000 na kondoo 10,000. Idadi kubwa ya makuhani walijitakasa.

25. Kila mtu aliyehudhuria alifurahi sana. Watu wote wa Yuda, makuhani na Walawi, wakazi wa Yerusalemu waliohudhuria, wageni waliotoka nje ya Yerusalemu na wale walioishi Yuda, wote walifurahi sana.

26. Kukawa na furaha kuu mno Yerusalemu, maana tangu enzi ya mfalme Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli, jambo kama hilo lilikuwa halijatokea Yerusalemu.

27. Kisha, makuhani na Walawi wakawaombea watu baraka zake Mwenyezi-Mungu, naye katika makao yake matakatifu huko mbinguni akayasikia maombi yao na kuyakubali.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 30