Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 30:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mfalme Hezekia aliwatumia ujumbe watu wote wa Israeli na Yuda, na pia akawaandikia barua wenyeji wa Efraimu na Manase, akiwaalika wote waje katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu Yerusalemu, ili kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka kwa heshima yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

2. Mfalme, viongozi na watu wote wa mji wa Yerusalemu waliafikiana kuiadhimisha sikukuu hiyo ya Pasaka mnamo mwezi wa pili

3. badala ya mwezi wa kwanza kama ilivyokuwa kawaida, kwa sababu idadi ya makuhani waliokuwa wamekwisha kujiweka wakfu ilikuwa ndogo, nao watu walikuwa bado hawajakusanyika Yerusalemu.

4. Aidha, mpango huu ulimridhisha mfalme pamoja na watu wote waliokuwa wamekusanyika.

5. Kwa hiyo waliamua kutoa tangazo kote nchini Israeli, kutoka Beer-sheba hadi Dani, kwamba watu waje Yerusalemu kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Ulikuwa umepita muda mrefu kabla watu hawajaiadhimisha Pasaka kulingana na sheria zake.

6. Matarishi, kwa amri yake mfalme na maofisa wake, walipeleka barua kote nchini Israeli na Yuda. Barua hizo zilikuwa na ujumbe ufuatao:“Enyi watu wa Israeli mlionusurika baada ya mashambulizi ya wafalme wa Ashuru. Mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Israeli, ili naye apate kuwarudieni.

7. Msiwe kama babu zenu na ndugu zenu ambao hawakuwa waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, ambaye kama mnavyoona aliwaadhibu vikali.

8. Msiwe wakaidi kama babu zenu, ila mtiini Mwenyezi-Mungu. Njoni katika hekalu lake ambalo amelitakasa milele, mumwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ili asiwakasirikie.

9. Mkimrudia Mwenyezi-Mungu, wale ambao waliwateka ndugu zenu na watoto wenu, watawahurumia na kuwaacha warudi katika nchi hii. Kwa maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni mwenye rehema na huruma, naye atawapokea ikiwa mtamrudia.”

10. Basi, matarishi hao wakaenda toka mji mmoja hadi mwingine kote nchini Efraimu na Manase, wakafika hata Zebuluni. Lakini watu waliwacheka na kuwadhihaki.

11. Hata hivyo, watu wachache miongoni mwa makabila ya Asheri, Manase na Zebuluni, walijinyenyekesha wakaja Yerusalemu.

12. Nguvu ya Mungu ilikuwa ikifanya kazi katika Yuda, akawapa moyo kutii amri za mfalme na maofisa wake kadiri ya maagizo ya Mwenyezi-Mungu.

13. Watu wengi sana walijumuika mjini Yerusalemu mnamo mwezi wa pili, kuiadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu.

14. Walianza kazi, wakaziondoa madhabahu zote zilizokuwa Yerusalemu, na nyingine zote zilizotumiwa kufukizia ubani, wakazibeba na kuzitupa katika Bonde la Kidroni.

15. Siku ya kumi na nne ya mwezi huo walichinja mwanakondoo wa Pasaka. Makuhani na Walawi waliona aibu, wakajitakasa na kuleta sadaka za kuteketeza katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

16. Walichukua nafasi zao hekaluni kulingana na maagizo yaliyokuwamo katika sheria za Mose, mtu wa Mungu. Walawi waliwapa makuhani damu ya tambiko, nao wakainyunyiza madhabahuni.

17. Kwa vile wengi wa wale waliokusanyika hapo hawakuwa wamejitakasa, iliwabidi Walawi kuwachinjia wanakondoo wa Pasaka na kuwaweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 30