Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 23:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Baadaye, mnamo mwaka wa saba, kuhani Yehoyada alijipa moyo akafanya mapatano na makapteni: Azaria mwana wa Yehoramu, Ishmaeli mwana wa Yehohanani, Azaria mwana wa Obedi, Maaseya mwana wa Adaya, na Elishafati mwana wa Zikri.

2. Wakazunguka katika miji yote ya Yuda wakiwakusanya Walawi na viongozi wa makabila ya Israeli, wakaenda mpaka Yerusalemu.

3. Mkutano wote ukafanya agano na mfalme katika nyumba ya Mungu. Yehoyada akawaambia, “Mwangalie huyu mwana wa mfalme! Mwacheni atawale kulingana na ahadi aliyoitoa Mwenyezi-Mungu kuhusu uzao wa Daudi.

4. Hivi ndivyo mtakavyofanya: Theluthi moja yenu nyinyi makuhani na Walawi mtakaoshika zamu siku ya Sabato, mtayalinda malango,

5. theluthi nyingine italinda ikulu na theluthi iliyobakia mtalinda Lango la Msingi. Watu wote watakuwa katika nyua za nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

6. Asikubaliwe mtu mwingine yeyote kuingia nyumba ya Mwenyezi-Mungu isipokuwa makuhani tu pekee na wale Walawi watakaokuwa wanahudumu. Hao wanaweza kuingia kwa sababu wao ni watakatifu, lakini wale watu wengine wote, watatii amri ya Mwenyezi-Mungu.

7. Walawi watamzunguka mfalme, kila mtu na silaha yake mkononi; na mtu yeyote atakayejaribu kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, atauawa. Mkae na mfalme popote aendapo.”

8. Walawi na watu wa Yuda walitii amri zote alizotoa kuhani Yehoyada. Kila ofisa akawachukua watu wake wote, wale waliokuwa wamemaliza zamu na wale waliokuwa wanaingia kushika zamu siku ya Sabato; kwa sababu Yehoyada hakuwaruhusu waondoke.

9. Kisha kuhani Yehoyada akawapa makapteni mikuki na ngao kubwa na ndogo zilizokuwa mali ya mfalme Daudi, na ambazo zilikuwa zimewekwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

10. Kisha, akawapanga watu wote kuanzia upande wa kusini mpaka upande wa kaskazini wa nyumba na kuzunguka madhabahu na nyumba, kila mmoja silaha yake mkononi, ili kumlinda mfalme.

11. Halafu wakamtoa nje mwana wa mfalme, wakamvika taji kichwani, na kumpa ule ushuhuda; wakamtawaza nao Yehoyada na wanawe wakampaka mafuta awe mfalme, kisha watu wakashangilia wakisema, “Aishi mfalme!”

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 23