Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 20:14-26 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Ndipo Roho wa Mwenyezi-Mungu akamjia mmoja wa Walawi aliyekuwa hapo, jina lake Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, wa ukoo wa Asafu.

15. Yahazieli akasema, “Sikilizeni watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu na mfalme Yehoshafati, Mwenyezi-Mungu awaambia hivi: Msiogope wala msihangaike kwa sababu ya jeshi hili kubwa. Vita hivi si vyenu, bali ni vya Mungu.

16. Kesho washambulieni wakati watakapokuwa wakipanda Bonde la Sisi. Mtawakuta mwisho wa bonde, mashariki mwa jangwa la Yerueli.

17. Hamtahitaji kupigana vita hivi. Nyinyi jipangeni tu halafu mngojee, na mtaona Mwenyezi-Mungu akiwashinda kwa niaba yenu. Enyi watu wa Yuda na Yerusalemu, msiogope wala msifadhaike. Nendeni vitani, naye Mwenyezi-Mungu atakuwa pamoja nanyi!”

18. Hapo mfalme Yehoshafati akasujudu pamoja na watu wote wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu wakamsujudu na kumwabudu Mwenyezi-Mungu.

19. Walawi wa ukoo wa Kohathi na Kora, wakasimama na kumsifu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa sauti kubwa sana.

20. Kesho yake, wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda mpaka katika jangwa la Tekoa. Walipokuwa wanaondoka, Yehoshafati alisimama, akawaambia, “Nisikilizeni, enyi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu! Mwaminini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nanyi mtakuwa imara. Muwe na imani na manabii wake, nanyi mtafaulu.”

21. Baada ya kushauriana na watu, mfalme alichagua wanamuziki fulani, akawaagiza wajivike mavazi yao rasmi kisha watangulie mbele ya jeshi, wakiimba:“Mshukuruni Mwenyezi-Mungu,maana fadhili zake zadumu milele!”

22. Wakati walipoanza kuimba na kusifu, Mwenyezi-Mungu aliwavuruga akili wanajeshi wa Amoni, Moabu na wa Mlima Seiri waliokuja kupigana na Yuda. Na wanajeshi hao wakashindwa.

23. Watu wa Amoni na wa Moabu wakawashambulia wenyeji wa mlima Seiri, na kuwaangamiza kabisa. Baada ya kuwaangamiza wakazi wa mlima Seiri wakaanza kushambuliana wao kwa wao, wakaangamizana.

24. Jeshi la Yuda lilipofika penye mnara wa ulinzi huko jangwani, waliangalia upande wa maadui, wakaona maiti zimetapakaa kila mahali. Hakuna mtu yeyote aliyenusurika.

25. Yehoshafati na wanajeshi wake wakaenda kuchukua nyara wakakuta ng'ombe wengi, mali, nguo na vitu vingine vya thamani. Iliwachukua muda wa siku tatu kusomba nyara hizo, na hata hivyo, hawakuzimaliza kwani zilikuwa nyingi mno.

26. Siku ya nne wakakusanyika katika Bonde la Sifa, na kumsifu Mwenyezi-Mungu kwa yote aliyowafanyia. Ndio maana bonde hilo linaitwa Bonde la Sifa hadi hivi leo.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 20