Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 2:7-16 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Basi, sasa nitumie mtu mwenye ujuzi wa kutengeneza vyombo kwa dhahabu, fedha, shaba, na chuma, na nguo za rangi ya zambarau, za rangi nyekundu na ya samawati, ajuaye pia, kutia nakshi. Yeye atashirikiana katika kazi hiyo na mafundi walioko pamoja nami katika Yuda na Yerusalemu, ambao baba yangu Daudi aliwachagua.

8. Tena nipelekee mierezi, miberoshi na misandali kutoka Lebanoni, kwa maana najua ya kwamba watumishi wako ni hodari sana wa kupasua mbao huko Lebanoni. Nao watumishi wangu watashirikiana na watumishi wako,

9. ili wanipasulie mbao kwa wingi, maana nyumba ninayokusudia kujenga ni kubwa na ya ajabu.

10. Kwa ajili ya watumishi wako, yaani maseremala watakaopasua mbao, nitatoa tani 2,000 za ngano iliyopondwa, tani 2,000 za shayiri, lita 400,000 za divai na lita 400,000 za mafuta.”

11. Naye Hiramu, mfalme wa Tiro, alimjibu Solomoni kwa barua akisema:“Kwa kuwa Mwenyezi-Mungu anawapenda watu wake, amekufanya uwe mfalme wao.

12. Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliyeziumba mbingu na dunia! Amempa mfalme Daudi mwana mwenye hekima, busara na akili, atakayemjengea Mwenyezi-Mungu nyumba, na kujijengea ikulu.

13. Sasa nakupelekea fundi stadi sana na mwenye akili, jina lake Huramu-abi,

14. mwana wa mmoja wa wanawake wa kabila la Dani, na baba yake alikuwa mkazi wa Tiro. Yeye ana ujuzi mwingi wa kutumia dhahabu, fedha, shaba, chuma, mawe, miti, rangi ya zambarau, ya samawati, nyekundu na nguo za kitani safi. Tena ni hodari na anaweza kutia nakshi na kuchora michoro ya kila aina kufuatana na kielelezo chochote ambacho angepewa. Yeye atafanya kazi pamoja na mafundi wako, mafundi wa bwana wangu, Daudi, baba yako.

15. Sasa basi, bwana wangu, vitu hivyo ulivyosema: Ngano, shayiri, mafuta na divai, tafadhali uvitume kwa watumishi wako,

16. nasi tutapasua mbao kadiri ya mahitaji yako kutoka huko Lebanoni; kisha tutazifunga pamoja zielee majini mpaka Yopa. Kutoka huko utazipeleka Yerusalemu.”

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 2