Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 17:8-18 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Walawi tisa na Makuhani wawili waliandamana nao. Walawi hao walikuwa Shemaya, Nethania, Zebadia, Asaheli, Shemiramothi, Yehonathani, Adoniya, Tobia na Tob-adoniya; na makuhani walikuwa Elishama na Yehoramu.

9. Walikichukua kitabu cha sheria ya Mwenyezi-Mungu, wakazunguka nacho katika miji yote ya Yuda wakifundisha watu.

10. Mwenyezi-Mungu alizitia hofu falme zote jirani na Yuda, zikaogopa kupigana vita na Yehoshafati.

11. Baadhi ya Wafilisti walimletea Yehoshafati zawadi pamoja na fedha nyingi, na Waarabu wengine nao wakamletea kondoo madume 7,700, na mabeberu 7,700.

12. Kwa hiyo Yehoshafati aliendelea kuwa mkuu zaidi. Alijenga ngome na miji yenye ghala,

13. kwa hiyo alikuwa na ghala kubwa katika miji ya Yuda. Huko Yerusalemu, aliweka askari wa jeshi mashujaa.

14. Hii ndiyo orodha yao kulingana na koo za baba zao: Adna alikuwa kamanda wa vikosi vya askari 1,000 wa kabila la Yuda. Chini yake, kulikuwa na askari laki tatu.

15. Wa pili katika cheo alikuwa kamanda Yehohanani, akiwa na askari 280,000,

16. na wa tatu alikuwa Amasia mwana wa Zikri, akiwa na askari mashujaa 200,000. Amasia alijitolea kwa hiari kumtumikia Mwenyezi-Mungu.

17. Kamanda wa vikosi vya askari, waliotoka katika kabila la Benyamini alikuwa Eliada, mtu shupavu, naye alikuwa na askari 200,000, wenye nyuta na ngao.

18. Wa pili alikuwa Yehozabadi, aliyekuwa na askari 180,000 waliojiandaa tayari kwa vita.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 17