Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 13:10-22 Biblia Habari Njema (BHN)

10. “Lakini kuhusu sisi, Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu wetu, wala hatujamwacha. Tena tunao makuhani wa uzao wa Aroni ambao wanamtumikia Mwenyezi-Mungu, nao husaidiwa na Walawi.

11. Kila siku asubuhi na jioni, makuhani humtolea sadaka za kuteketezwa nzima, na kumfukizia ubani wenye harufu nzuri, tena hupanga juu ya meza ya dhahabu safi, mikate ya kuwekwa mbele ya Mungu, na kukitunza kinara cha dhahabu na kuziwasha taa kila siku jioni. Sisi tunayafuata maagizo ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, lakini nyinyi mmemwacha.

12. Hebu tazameni, Mungu mwenyewe ndiye kiongozi wetu na makuhani wake wanazo tarumbeta zao tayari kuzipiga ili kutupa ishara ya kuanza vita dhidi yenu. Enyi watu wa Israeli, acheni kupigana vita dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu. Hamwezi kushinda!”

13. Lakini wakati huo, Yeroboamu alikuwa amekwisha tuma baadhi ya wanajeshi wake kulivamia jeshi la Yuda kutoka upande wa nyuma, hali wale wengine wamewakabili kutoka upande wa mbele.

14. Watu wa Yuda walipotazama nyuma, walishtuka kuona wamezingirwa; basi walimlilia Mwenyezi-Mungu, nao makuhani wakazipiga tarumbeta zao.

15. Ndipo wanajeshi wa Yuda wakapiga kelele ya vita, na walipofanya hivyo, Mungu alimshinda Yeroboamu na jeshi lake la watu wa Israeli mbele ya Abiya na watu wa Yuda.

16. Watu wa Israeli waliwakimbia watu wa Yuda naye Mungu akawatia mikononi mwao.

17. Abiya na jeshi lake aliwashambulia sana, akawashinda; akaua wanajeshi wa Israeli, laki tano waliokuwa baadhi ya wanajeshi hodari sana katika Israeli.

18. Kwa hiyo, watu wa Yuda walipata ushindi dhidi ya watu wa Israeli kwa sababu walimtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao.

19. Abiya alimfukuza Yeroboamu, akamnyanganya baadhi ya miji yake: Betheli, Yeshana, Efroni pamoja na vijiji vilivyokuwa kandokando ya miji hiyo.

20. Yeroboamu hakuweza kupata nguvu tena wakati wa Abiya. Mwishowe Mwenyezi-Mungu alimpiga, naye akafa.

21. Lakini Abiya aliendelea kupata nguvu zaidi. Akaoa wanawake kumi na wanne, akapata watoto wa kiume ishirini na wawili na mabinti kumi na sita.

22. Matendo mengine ya Abiya, shughuli zake na maneno yake, yameandikwa katika kitabu cha “Historia ya Nabii Ido.”

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 13