Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 13:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Abiya alianza kutawala Yuda mnamo mwaka wa kumi na nane wa utawala wa mfalme Yeroboamu.

2. Alitawala kwa muda wa miaka mitatu akiwa Yerusalemu. Mama yake alikuwa Maaka binti Urieli wa Gibea.Kulitokea vita kati ya Abiya na Yeroboamu.

3. Abiya alijiandaa kupigana vita akiwa na jeshi la askari hodari 400,000, naye Yeroboamu akamkabili na jeshi lake la askari hodari 800,000.

4. Mfalme Abiya alisimama juu ya mlima Semaraimu, ulioko kati ya milima ya Efraimu, akamwambia Yeroboamu na watu wa Israeli, “Nisikilize ewe Yeroboamu na watu wote wa Israeli!

5. Je, hamjui kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, alimwahidi Daudi kwa kufanya naye agano lisilovunjika kuwa daima, wafalme wote wa Israeli watatoka katika uzao wake?

6. Lakini Yeroboamu mwana wa Nebati mtumishi wa Solomoni, mwana wa Daudi alimwasi bwana wake.

7. Baadaye, alijikusanyia kikundi cha mabaradhuli, watu wapumbavu wasiofaa kitu, nao wakamshawishi Rehoboamu mwana wa Solomoni, kutenda yale waliyotaka wao, naye hangeweza kuwazuia kwani wakati huo alikuwa bado kijana bila uzoefu mwingi.

8. “Sasa nyinyi mnadhani mnaweza kupinga ufalme wa Mwenyezi-Mungu aliopewa Daudi na uzao wake kwa sababu eti mnalo jeshi kubwa na sanamu za dhahabu za ndama, alizowatengenezea Yeroboamu kuwa miungu yenu!

9. Je, hamkuwafukuza makuhani wa Mwenyezi-Mungu, wana wa Aroni, kadhalika na Walawi, na kujifanyia makuhani wenu wenyewe kama wafanyavyo watu wa mataifa mengine? Yeyote ajaye kwenu kujiweka wakfu na ndama dume ama kondoo madume saba, huwa kuhani wa vitu ambavyo si miungu.

10. “Lakini kuhusu sisi, Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu wetu, wala hatujamwacha. Tena tunao makuhani wa uzao wa Aroni ambao wanamtumikia Mwenyezi-Mungu, nao husaidiwa na Walawi.

11. Kila siku asubuhi na jioni, makuhani humtolea sadaka za kuteketezwa nzima, na kumfukizia ubani wenye harufu nzuri, tena hupanga juu ya meza ya dhahabu safi, mikate ya kuwekwa mbele ya Mungu, na kukitunza kinara cha dhahabu na kuziwasha taa kila siku jioni. Sisi tunayafuata maagizo ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, lakini nyinyi mmemwacha.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 13