Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 1:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Solomoni, mwanawe mfalme Daudi, alijiimarisha katika utawala wake, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wake alikuwa pamoja naye, akambariki na kumfanya awe mkuu sana.

2. Mfalme Solomoni aliwaita makamanda wote wa vikosi vya maelfu na vya mamia, waamuzi, na viongozi wote wa koo za Israeli.

3. Kisha akaandamana nao hadi mahali pa ibada huko Gibeoni. Walikwenda huko kwa sababu hapo ndipo mahali lilipokuwa hema la mkutano la Mungu alilolitengeneza Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, nyikani.

4. (Lakini, sanduku la Mungu lilikuwa Yerusalemu katika hema ambalo mfalme Daudi alilipigilia alipolileta kutoka Kiriath-yearimu).

5. Tena, madhabahu ya shaba iliyotengenezwa na Bezaleli, mwana wa Uri na mjukuu wa Huri, pia ilikuwa huko Gibeoni mbele ya hema takatifu la Mwenyezi-Mungu. Hapo mfalme Solomoni na watu wote wakamwomba Mwenyezi-Mungu.

6. Solomoni alipanda mbele ya madhabahu ya shaba iliyokuwa kwenye hema la mkutano. Hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu, akatoa tambiko 1,000 za kuteketezwa juu ya madhabahu hayo.

7. Usiku huo, Mungu alimtokea Solomoni, akamwambia, “Omba chochote, nami nitakupa.”

8. Solomoni akamwambia Mungu, “Ulimwonesha baba yangu Daudi fadhili nyingi, na umenijalia kuwa mfalme mahali pake.

9. Sasa, ee Mungu, Mwenyezi-Mungu, itimize ahadi uliyompa baba yangu Daudi. Umenitawaza niwe mfalme juu ya watu hawa walio wengi kama mavumbi.

10. Kwa hiyo, nakuomba unipe hekima na maarifa ili niweze kuwatawala watu wako vizuri. La sivyo, nitawezaje kuwatawala hawa watu wako walio wengi hivi?”

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 1