Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 22:9-16 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Basi, Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwita mtumishi mmoja, akamwamuru, “Haraka! Nenda ukamlete Mikaya mwana wa Imla.”

10. Wakati huo, mfalme wa Israeli pamoja na Yehoshafati mfalme wa Yuda, walikuwa wameketi katika viti vyao vya enzi wakikaa kwenye kiwanja cha kupuria nafaka kwenye lango la kuingilia mjini Samaria nao walikuwa wamevalia mavazi yao ya kifalme; wakati huo manabii wote wakawa wanatabiri mbele yao.

11. Kisha mmoja wa manabii hao, Sedekia mwana wa Kenaana, akajitengenezea pembe za chuma akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa pembe hizi, utawarudisha nyuma Waaramu na kuwaangamiza.’”

12. Hata wale manabii wengine wote wakatabiri vivyo hivyo, wakasema, “Nenda uushambulie Ramoth-gileadi, utashinda! Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.”

13. Wakati huo, yule mtumishi aliyetumwa kwenda kwa Mikaya, alimwambia, “Manabii wengine wote kwa pamoja, wamemtabiria mfalme ushindi; tafadhali, nawe pia ufanye kama wao, umtabirie mema.”

14. Lakini Mikaya akamjibu, “Ninaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, mimi nitasema tu yale atakayoniambia Mwenyezi-Mungu.”

15. Basi, Mikaya alipofika mbele ya mfalme, mfalme alimwuliza, “Je, twende kupigana vita huko Ramoth-gileadi ama tusiende?” Naye alimjibu, “Nenda na ufanikiwe, naye Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.”

16. Lakini mfalme akamwambia, “Nitakuapisha mara ngapi kwamba unaposema nami kwa jina la Mwenyezi-Mungu, ni lazima uniambie ukweli mtupu?”

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 22