Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 18:7-24 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Obadia alipokuwa njiani, alikutana na Elia; naye Obadia alipomtambua Elia, aliinama chini na kusema, “Kumbe! Ni wewe bwana wangu Elia?”

8. Elia akamwambia, “Naam! Ni mimi Elia. Nenda ukamwambie bwana wako kwamba niko hapa.”

9. Obadia akasema, “Nimekosa nini hata utake kunitia hatarini ili niuawe na mfalme Ahabu?

10. Nakuapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wako aliye hai, kwamba mfalme amekuwa akikutafuta duniani kote. Na mfalme yeyote akisema kwamba hujaonekana huko, Ahabu alimtaka huyo mfalme aape na watu wake kwamba kweli hupo.

11. Na sasa, wataka niende kumwambia kwamba wewe uko hapa!

12. Ninahofia kwamba mara nitakapoondoka, Roho ya Mwenyezi-Mungu itakunyakua na kukupeleka mahali nisipopajua! Nikienda kumwambia Ahabu kwamba uko hapa, naye akikutafuta asikupate, ataniua mimi, ingawaje mimi mtumishi wako nimemcha Mwenyezi-Mungu tangu ujana wangu.

13. Je, huna habari kwamba Yezebeli alipokuwa akiwaua manabii wa Mwenyezi-Mungu, mimi niliwaficha manabii 100, watu hamsinihamsini pangoni, nikawa nawapa chakula na maji?

14. Sasa waniambia ati niende kumwambia bwana wangu kwamba wewe Elia uko hapa! Ahabu ataniua.”

15. Elia akamwambia, “Nakuapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa Majeshi, aishivyo ambaye ninamtumikia: Leo hii nitajitokeza mbele ya mfalme.”

16. Basi, Obadia akaenda kwa mfalme Ahabu, akampa habari hizo. Naye Ahabu akaenda kukutana na Elia.

17. Ahabu alipomwona Elia, alisema, “Kumbe kweli ni wewe, mtaabishaji wa Israeli?”

18. Elia akamjibu, “Mtaabishaji wa Israeli si mimi, bali ni wewe na jamaa ya baba yako. Nyinyi mmekiuka amri za Mwenyezi-Mungu na kuabudu Mabaali.

19. Sasa, uwakusanye watu wote wa Israeli mbele yangu huko mlimani Karmeli. Hali kadhalika, wakusanye wale manabii 450 wa Baali, na manabii 400 wa Ashera mungu wa kike, ambao huhifadhiwa na malkia Yezebeli.”

20. Basi, Ahabu akawaita watu wote wa Israeli, akawakusanya na manabii wote kule mlimani Karmeli.

21. Kisha, Elia akawakaribia watu hao, akawaambia, “Mtasitasita na kuyumbayumba mioyoni mpaka lini? Ikiwa Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu mfuateni; lakini ikiwa Baali ni Mungu, basi, mfuateni yeye.” Lakini watu hawakumjibu neno lolote.

22. Hapo, Elia akawaambia, “Mimi tu ndiye peke yangu nabii wa Mwenyezi-Mungu niliyebaki, lakini manabii wa Baali wapo 450.

23. Haya! Leteni fahali wawili; manabii wa Baali wajichagulie fahali mmoja, wamchinje, wamkate vipandevipande na kumweka juu ya kuni, bila kuwasha moto. Nami pia nitamtwaa huyo fahali mwingine, nitamchinja na kumweka juu ya kuni bila kuwasha moto.

24. Kisha, wao watamwomba mungu wao, nami nitamwomba Mwenyezi-Mungu. Mungu atakayejibu kwa kuleta moto, huyo ndiye Mungu wa kweli.” Na hapo umati wote ukasema, “Naam! Na iwe hivyo.”

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 18