Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 18:32-42 Biblia Habari Njema (BHN)

32. Kwa mawe hayo, Elia alimjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu, akachimba na mtaro kuizunguka madhabahu hiyo; mtaro uwezao kuchukua kama debe moja na nusu la nafaka.

33. Kisha akapanga kuni vizuri, akamkata vipandevipande yule fahali, akaviweka juu ya kuni. Kisha akawaambia watu, “Jazeni mitungi minne maji mkaimwagie tambiko hii ya kuteketezwa pamoja na kuni.” Wakafanya hivyo.

34. Kisha akawaambia, “Rudieni tena.” Nao wakafanya hivyo mara ya pili. Naye akawaambia, “Fanyeni hivyo tena mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo.

35. Maji yakatiririka chini pande zote za madhabahu, hata yakajaa mtaroni.

36. Mnamo alasiri, wakati wa kutoa tambiko, nabii Elia aliikaribia madhabahu, akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, waoneshe watu leo hii kwamba wewe ndiwe Mungu wa Israeli, na kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya kwa amri yako.

37. Unijibu, ee Mwenyezi-Mungu; unijibu ili watu hawa wajue kuwa wewe Mwenyezi-Mungu ndiwe Mungu, na kwamba umeigeuza mioyo yao wakurudie.”

38. Mara, Mwenyezi-Mungu akashusha moto, ukaiteketeza tambiko hiyo ya kuteketezwa, kuni, mawe na vumbi, na kuyakausha maji yote mtaroni.

39. Watu walipoona hivyo, walianguka kifudifudi na kusema, “Mwenyezi-Mungu, ni Mungu; Mwenyezi-Mungu, ni Mungu!”

40. Ndipo Elia akawaambia, “Wakamateni manabii wote wa Baali. Msimwache hata mmoja wao atoroke!” Basi, watu wakawakamata wote, naye Elia akawapeleka mtoni Kishoni, akawaulia huko.

41. Baada ya hayo, Elia akamwambia mfalme Ahabu, “Nenda ukale na kunywa. Nasikia kishindo cha mvua.”

42. Basi, Ahabu akaenda zake kula na kunywa; naye Elia akapanda juu ya kilele cha mlima Karmeli, na huko akainama hadi chini na kuuweka uso wake katikati ya magoti yake.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 18