Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 15:25-34 Biblia Habari Njema (BHN)

25. Mnamo mwaka wa pili wa utawala wa Asa huko Yuda, Nadabu, mwana wa Yeroboamu, alianza kutawala huko Israeli. Alitawala kwa muda wa miaka miwili.

26. Nadabu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; akamwiga baba yake ambaye aliwafanya watu wa Israeli watende dhambi.

27. Baasha mwana wa Ahiya, wa kabila la Isakari, akala njama dhidi ya Nadabu. Basi, wakati Nadabu na jeshi lake walipokuwa wameuzingira mji wa Gibethoni wa Wafilisti, Baasha akamvamia na kumwua,

28. akatawala mahali pake. Huo ulikuwa mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Asa wa Yuda.

29. Mara tu alipoanza kutawala, Baasha akawaua watu wote wa jamaa ya Yeroboamu; hakuacha hai hata mtu mmoja wa jamaa ya Yeroboamu; hiyo ilikuwa sawa na yale aliyosema Mwenyezi-Mungu kwa njia ya mtumishi wake, Ahiya wa Shilo.

30. Mambo haya yalifanyika kwa sababu Yeroboamu alimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa dhambi yake na kwa kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi.

31. Matendo mengine ya Nadabu, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli.

32. Mfalme Asa wa Yuda na mfalme Baasha wa Israeli walikuwa na vita kati yao wakati wote walipokuwa wakitawala.

33. Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Baasha mwana wa Ahiya, alianza kutawala Israeli kutoka Tirza. Alitawala kwa muda wa miaka ishirini na minne.

34. Baasha alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamwiga Yeroboamu na kutenda dhambi ileile ambayo aliwafanya watu wa Israeli watende.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 15